Baada ya Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Kiafrika ya mwaka 2017 inayotolewa kwa wandishi bora katika vitengo vya ushairi na Riwaya kupokezwa Dotto Rangimoto na Ali Hilal Bilal jijini Nairobi, wawili hao kutoka Tanzania wanaeleza kuwa msukumo wa kuandika kwa kutumia lugha ya Kiswahili ndio uliokuwa chachu yao kujizolea tuzo hizo.
Tuzo hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya Mabati Rolling Mills na Chuo Kikuu cha Cornell cha Marekani hutolewa kila mwaka kwa vitabu bora katika fani ya riwaya na ushairi.
Malengo ya tuzo hii iliyoanzishwa mwaka 2014 jijini Nairobi na Dkt Lizzy Attree, Mkurugenzi wa Tuzo ya Caine na Professa Mukoma wa Ngugi, kutoka Chuo Kikuu cha Cornell nchini Marekani, ni kuthamini uandishi wa lugha za kiafrika na vile vile kutafsiri lugha nyingine kwa lugha za kiafrika.
Dotto Rangimoto alishinda kwenye kitengo cha ushairi kwa mswada wake Mwanangu Rudi Nyumbani huku Ali Hilal Ali akiibuka kidedea katika kitengo cha riwaya kwa mswada wake Mmeza fupa na kupokezwa kima cha $5,000 kila mmoja.
Dotto Rangimoto, akizungumza na Idhaa ya Sauti ya Amerika jijini Nairobi, hakuficha furaha yake kwa kushinda tuzo kwa kitengo cha ushairi.
Ali Hilal Ali aliyetuzwa kupitia kitengo cha riwaya naye anaeleza kuwa kutuzwa huku kunampa matumaini sana ya kuandika zaidi maanake Kiswahili kinalipa.
Professa Abdilatif Abdalla ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell anaelezea vigezo vinavyomfanya mwandishi bora kutuzwa.
Professa Mukoma wa Ngugi mojawapo wa waasisi wa Tuzo hii anaeleza kuwa kutuzwa huku kwa wandishi wa Tanzania ni changamoto kwa wandishi wa Kenya kuandika zaidi.
Aidha, Professa Iribe Mwangi Mwenyekiti wa Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Nairobi naye ansema kuwa upo umuhimu mkubwa wa tuzo hii kwa watu wanaoishi barani Afrika.
Baada ya Dotto Rangimoto na Ali Hilal Ali kutangazwa washindi, waziri wa Tanzania wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe aliwapongeza wawili hao kwa kupeperusha bendera ya taifa hilo na vile vile kuimarisha utamaduni wa taifa kupitia lugha ya Kiswahili.
Baadhi ya waliohudhuria hafla hiyo ni aliyekuwa jaji mkuu wa Kenya, Willy Mutunga ambaye aliwakabidhi hundi washindi wa shindano hilo.
Washindi hao walipokea $5,000 kila mmoja.
- Ripoti hii imeandikwa na mwanahabari wa VOA Kennedy Wandera akiwa Nairobi