Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Juni 19, 2024 Local time: 20:38

Wanawake wa Kiafrika kupokea Tuzo ya Kimataifa ya Wanawake Mashujaa


Roegchanda Pascoe(Courtesy photo)
Roegchanda Pascoe(Courtesy photo)

Roegchanda Pascoe alionyesha ushujaa kukabiliana na vitisho vya kuuawa wakati akijaribu kuzuia ghasia za magenge zilizokuwa zimezikumba jamii za makazi ya Cape nje kidogo ya mji wa Cape Town, Afrika Kusini. Facia Boyenoh Harris alikabiliwa na manyanyaso wakati akitetea haki za wanawake na ulinzi wa unyanyasaji wa kingono nchini Liberia

Wanawake hawa wawili Waafrika kutoka nchi zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara ni kati ya darzeni za wanawake wanaopewa heshima na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani na Tuzo ya Kimataifa ya Wanawake Mashujaa kwa kuonyesha “ujasiri usio wa kawaida, nguvu na uongozi katika kupigania amani, haki, haki za binadamu, uwiano wa kijinsia, na usawa … mara nyingi kwa kuweka maisha yao hatarini na kujitoa mhanga,” kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari.

Watatambuliwa Jumatatu katika hafla ambayo, kutokana na janga la corona, itawaleta wote hao pamoja kwa njia ya mtandao badala ya kuhudhuria binafsi mjini Washington. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken ataongoza tafrija hiyo, na mke wa Rais Jill Biden atatoa hotuba.

Roegchanda Pascoe

Pascoe, mwenye umri wa miaka 47, ni mwanaharakati anayefanya kazi kuzuia uhalifu katika nyumba za Cape, jamii maskini nje ya mji wa Cape Town ambako watu wa makabila mbalimbali walilazimishwa kukaa eneo hilo katika miaka 1960 chini ya mfumo wa utawala wa kibaguzi Afrika Kusini.

Magenge yamekuwa na makazi yao kwa miongo mingi hapo, wakisafirisha dawa za kulevya, silaha, ukahaba na mengine mengi. Ghasia zimefanywa “kuwa ni kitu cha kawaida,” Pascoe aliiambia VOA.

Lakini mwaka 2013, baada ya mvulana mmoja aliyekuwa akicheza nje aliuawa katika mapambano ya risasi, mwanamama huyu alikuwa muasisi mwenza wa Kikundi cha kujitolea cha Usalama cha Manenberg. Kilipewa jina la kitongoji ambapo kipo, Kikundi hicho kinatoa elimu kuhusu mfumo wa kisheria wa uhalifu, kinawapatia mafunzo watetezi wa kisheria wa kijamii, na kutoa ushauri nasaha na misaada mingine kwa waathirika wa uhalifu, hususan wanawake na watoto. Pascoe anapata posho kupitia mfuko wa msaada kutoka Kikundi cha Kimataifa Kinachopambana na Uhalifu Kimataifa (Global Initiative Against Transnational Organized Crime).

Kikundi hicho pia kinafanya usuluishi kati ya magenge mbalimbali, kwa lengo la kutafuta suluhu ya amani kwa mizozo.

Mwezi Julai 20, 2016, Pascoe na wakazi wengine kadhaa wa Manenberg walishuhudia madai ya shambulizi la genge dhidi ya mwanamme mmoja ambaye alikufa baadaye siku hiyo. Pascoe alikuwa ndiye shuhuda pekee kutoa ushahidi katika kesi ya mauaji ya mwaka 2019, akisaidia kumtia hatiani kiongozi wa genge hilo na wengine wawili.

Siku moja kabla ya kutoa ushuhuda, washambuliaji wasiojulikana walipiga risasi katika nyumba yake. Pascoe alikuwa amehamishiwa katika nyumba usalama mapema siku hiyo, lakini watoto wake walikuwa bado wako nyumbani. Tangu wakati huo wameungana naye mafichoni, wakihofia kulipiziwa kisasi na magenge hayo.

“Siwezi kukaa kimya wakati dhulma inatokea kwa kiumbe yeyote,” mwanamama huyo aliiambia VOA juu ya uamuzi wake wa kutoa ushahidi. Lakini “athari za ghasia za magenge zimekuwa mbaya sana kwangu mimi. … Sitaweza kurejea kuishi katika jamii hiyo.

Hata hivyo Pascoe amekuwa mvumilivu. Kupitia kikundi hicho, anaendelea kusuluhisha migogoro ya jamii na kuwasaidia waathirika wanawake na familia mbalimbali. Ameandaa program ya kuzuia na kuingilia kati matukio ya kihalifu kwa vijana walio kaitka mazingira hatarishi. Ameandaa mfumo wa “walking bus” kwa wanafunzi kusindikizwa na wazazi wao – aghlabu mama zao ambao hawana kazi. Wanalipwa, “wanafundishwa na kupewa ujuzi wa namna ya kutoa huduma ya kwanza dharura,” Pascoe amesema.

“Ana mikakati ya kustaajabisha ya kuiendeleza jamii yake,” Oscar Nceba Siwali amesema kuhusu Pascoe kupitia barua pepe aliyoituma VOA. Anaongoza Shirika la Afrika Kusini la Maendeleo na Ujenzi Mpya, linalohamasisha kujiepusha na ghasia katika baadhi ya jamii zilizoimara nchini humo.

“Katika warsha za kuzisaidia kuzihusisha taasisi zisizo za kiserikali kufanya kazi pamoja, amekuwa ni msaada mkubwa sana – anaelekeza jinsi ya kusonga mbele lakini pia anakiri [yale] yaliyopita.”

Pascoe anatarajia kuchaguliwa kwake kwa tuzo ya Mwanamke Jasiri itawasaidia wengine kutambua kuwa, haijalishi namna ulivyokuwa nyuma, wanaweza kutoa michango yenye kuthaminiwa.

“Itakuwa na maana kubwa sana kwa viongozi vijana wanawake,” amesema.

Facia Boyenoh Harris

Facia Boyenoh Harris mwanzilishi mwenza wa kikundi cha wanawake, Paramount Young Women Initiative Hivi leo, kinaendelea kutoa nafasi salama kuwasaidia watoto wa kike na wanawake vijana, kuhamasisha elimu, kutoa ushauri na uongozi. Monrovia, Liberia. (Photo courtesy of U.S. State Department)
Facia Boyenoh Harris mwanzilishi mwenza wa kikundi cha wanawake, Paramount Young Women Initiative Hivi leo, kinaendelea kutoa nafasi salama kuwasaidia watoto wa kike na wanawake vijana, kuhamasisha elimu, kutoa ushauri na uongozi. Monrovia, Liberia. (Photo courtesy of U.S. State Department)

Mwaka 2005, Harris alikuwa katika mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha African Methodist Episcopal katika mji mkuu wa Liberia, Monrovia, wakati yeye na baadhi ya wanafunzi wenzake walipoanzisha kikundi cha Vijana Wanawake, Paramount Young Women Initiative. Walichangisha fedha kwa ajili ya udhamini wa masomo kuwasaidia wanafunzi wengine wanaohangaika kupata fedha, majukumu ya kifamilia, matatizo ya masomo na mengine mengi.

Waliongeza warsha. “Tulizungumza kuhusu maisha ya familia, masuala ya uchumi wa jamii na uhamaishaji tunaohitaji” wakati Liberia ilipokuwa inaondokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, alisema Harris, mwenye umri wa miaka 39. “Tulikuwa na sehemu salama ya kukutana pamoja.”

Hivi leo, juhudi hizo zisizokuwa za kibiashara zinaendelea kutoa nafasi salama kuwasaidia watoto wa kike na wanawake vijana, kuhamasisha elimu, kutoa ushauri na uongozi.

Ni kituo kimoja cha wanaharakati kwa Harris, ambaye ni mwandishi wa zamani nchini Liberia, ambayo ina wajibu wa kuongoza juhudi za kuifikia jamii inayoendeshwa na Tume Huru ya Habari ya Liberia. Imepewa jukumu kutekeleza Sheria ya Uhuru wa Habari nchini.

Harris muasisi mwenza wa Kikundi cha Wanawake Liberia na, kama msimamizi wa kijamii, amekuwa akifanya kampeni kupanua wigo wa ushiriki wa kisiasa na hali bora ya usafi. Anapambana na manyanyaso ya kijinsia, ikiwemo ubakaji na ukeketaji wa wanawake.

Nchini Liberia, “tunakabiliana na mfumo dume wenye nguvu kubwa ambao unawakandamiza wanawake,” Harris alisema.

Rais wa Liberia alitangaza mwaka 2020 ubakaji ni dharura ya kitaifa, na serikali hivi karibuni ilianzisha mawasiliano mubashara ya simu katika kutoa taarifa za uhalifu wa kingono na kijinsia.

Lakini Waziri wa Jinsia Williametta E. Saydee-Tarr, akihutubia Baraza la Seneti la taifa Alhamisi [Machi10], alilalamika juu ya viwango vidogo vya kuripoti na kasi ya pole pole kwa mashtaka ya uhalifu huo.

“Kuna changamoto nyingi katika mfumo huo,” Harris alisema. Polisi mara nyingine wanasema hawana uwezo wa kuchunguza au kufanya ukamataji, au muathirika au ndugu zao hawataki kufungua mashtaka. Kesi zinaweza kukwama katika mfumo wa kukabiliana na uhalifu.

Watu wanahitaji “kupata haki kwa wakati,” Harris alisema.

Pia anatetea kuwepo uwakilishi sawa katika ofisi za umma. Ingawaje Liberia ilikuwa nchi ya kwanza Afrika kumchagua rais mwanamke – Ellen Johnson Sirleaf, rais aliyehudumu tangu mwaka 2006 hadi 2018 – wanawake bado uwakilishi wao uko chini katika ofisi za kuchaguliwa kitaifa. Harris ameeleza kuwa Bunge la Liberia, wanawake wana viti 11 kati ya 103 katika Baraza la Wawakilishi na Seneti wawili katika Baraza la Seneti lenye viti 30.

“Wanawake hawana fursa ya kupata fedha sawa” kwa kulipa ada na kampeni, alisema Harris, akipendekeza kuwepo na hatua za kuwawezesha kupata fedha za kampeni.

Harris alisema Tuzo ya Ushujaa inawaenzi “ wanawake wa Liberia ambao wamekuwa wakiendelea kufanya kazi ngumu kuhakikisha kuwa ukosefu wa haki unamalizwa” wakati wakiendeleza maendeleo ya nchi.

Inawakilisha changamoto binafsi, pia: “Nina majukumu makubwa zaidi kufanya zaidi … kuiacha Liberia bora kwa vizazi vitakavyokuja baada ya sisi.

Programu ya uongozi

Zaidi ya sherehe za tuzo zitakazo fanyika kwa njia ya mtandao Jumatatu, mashujaa hao watashiriki katika programu ya uongozi ya kupitia mtandaoni “ kuungana na wenzao wa Marekani na kuimarisha mtandao huo wa kimataifa wa viongozi wanawake,” Wizara ya Mambo ya Nje imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari. Zaidi wa wanaweka 170 kutoka nchi zaidi ya 80 wametambuliwa kutokana na kazi zao tangu mwaka 2007.

XS
SM
MD
LG