Wadau waliohudhuria mkutano wa pili wa kimataifa kuhusu kutokomeza ukeketaji wa wanawake, uliofanyika jijini Dar es salaam, wamesema utolewaji kwa mapana wa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji ndiyo suluhisho sahihi litakalotokomeza vitendo hivyo barani Afrika.
Mmoja wa waliohudhuria mkutano huo Sentamim Mussa kutoka Kenya amesema serikali za Afrika zinapaswa kubadilisha mitaala ya elimu ili kuwasaidia watoto kufahamu madhara ya ukeketaji.
Akitoa wito, Prisca Ngwashemi Mkurugenzi wa Taasisi ya Himiza Development Organization kutoka Pwani alisema wanaume wana nafasi kubwa ya kumaliza ukeketaji kwa kuwa huona kasoro na mapungufu kwa wanawake waliokeketwa hivyo wanapaswa kusimama kupinga utaratibu huo.
“Kina baba wainuke sasa wajitambue wao ndio wanatakiwa wawe msitari wa mbele kusisitiza kwamba swala la ukeketaji lisiwepo ili watoto wao wasikataliwe na wanaume”
Na kuongeza “kinachofanyika sasa hivi wanaume wa makabila yanayofanya ukeketaji wanaoa wanawake wa makabila ýao kama kifaa fulani tu halafu anakwenda kutafuta mwanamke mwingine wa kabila jingine. Na kuongezea kuwa mwanamme anamuona mke wake ana mapungufu, lakini ikiwa wanaume wanaelimishwa kuhusu ukeketaji basi utaondoka.”
Zaidi ya wanawake na wasichana millioni 68 wapo kwenye hatari ya kukeketwa duniani, wakati idadi barani Afrika ikiwa ni zaidi ya millioni 50. Kiwango ambacho kinaonyesha haja ya kufanya mabadiliko katika nchi za Afrika.
Akizungumza katika mkutano huo waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wadau kushirikiana na viongozi wa kimila, kidini, taasisi zisizo za kiserikali na jamii kuungana pamoja katika kutafuta suluhisho la kudumu la ukeketaji barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Mkutano huo ambao ulikuwa na kauli mbiu "Mabadiliko katika kizazi kimoja kwenda kingine ni muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukeketaji" umehudhuriwa na mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika ikiwemo Misri, Ethiopia, Gambia, Ghana pamoja na nchi kutoka mabara mengine.
Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.
Forum