Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 17, 2024 Local time: 21:04

Wananchi wa Tanzania waisihi serekali yao kutoa elimu zaidi ya homa ya Ini


Wadau wa afya wakiwa katika siku ya maadhimisho ya Homa ya Ini nchini Tanzania.
Wadau wa afya wakiwa katika siku ya maadhimisho ya Homa ya Ini nchini Tanzania.

Wakati Dunia inaadhimisha Siku ya Homa ya Ini wananchi wa Tanzania wamelalamikia kukosekana kwa elimu juu ya ugonjwa huo, hali ambayo inasababisha watu wengi kushindwa kufahamu namna ya kujikinga.

Wataalamu wa afya wameitaka serikali kushirikiana na wadau kuhakikisha elimu na chanjo zinatolewa vijijini na mijini ili kuepuka maambukizi mapya.

Wananchi hao wanasema kukosekana kwa elimu kunasababisha wengi wao kuchelewa kugundua na kutibu ugonjwa na kuufanya usambae na kusababisha ongezeko la maambukizi. Pia wananchi wengi wanashindwa kufahamu namna ya kujilinda dhidi ya ugonjwa huo.

Veronica Sando kutoka mkoani Mara ameitaka serikali kupeleka elimu kuhusiana na homa ya Ini katika maeneo ya vijijini ili kusaidia wananchi kufahamu ugonjwa huo na namna ya kujikinga.

“Ugonjwa wa ini kwakweli siwezi kusema kama nina elimu nao isipokuwa nasikia tu kwamba kuna ugonjwa wa ini na matatizo yake ni makubwa sana, wito wangu kwa serikali ni kwamba ijaribu kupeleka elimu hii chini hasa kwa wananchi walioko vijijini wasiotambua elimu hii na wasiofahamu kwamba kuna ugonjwa kama huu.” alisema Sando

Kutokana na uelewa mdogo wa ugonjwa huo, asilimia kubwa ya wananchi hawajapata chanjo ambayo hutolewa kwa malipo kwa watu wazima. Hali hii inaendelea kuwa tishio la kusambaa kwa maambukizi. Huku takwimu zikinaonyesha takribani Watanzania milioni moja wanakabiliwa na virusi vinavyosababisha homa ya ini aina ya B na C.

Bendi ya polisi wa Tanzania ikishiriki katika siku ya Homa ya Ini
Bendi ya polisi wa Tanzania ikishiriki katika siku ya Homa ya Ini

Elichilia Shao mtaalamu wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya KCMC Kilimanjaro, amesema ili kusaidia kupunguza changamoto ya maambukizi ya ugonjwa huo, serikali na wadau wanapaswa kutengeneza mfumo ambao utasaidia kuongeza wigo wa utoaji wa chanjo katika maeneo ya vijijini.

Ameongezea kusema Shayo “Kwa wale ambao wapo kwenye kaya ambazo hazina kipato cha kupata hata milo miwili au mitatu kwa siku, kungeweza kupatikana msaada kupitia programu mbalimbali ambazo zinahusisha pia mashirika mengine yasiyo ya kiserikali. Labda ingesaidia kuongeza wigo wa watu kupata chanjo ili baadaye tuwe na wananchi ambao hawana virusi vya homa ya ini aina ya B.”

Hata hivyo Dkt. Salimu Ismaili kutoka Hospitali ya Mkoa Geita ameitaka serikali kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu kuhusu ugonjwa huo, huku akishauri serikali kutumia njia za mawasiliano na mitandao ya kijamii kuhakikisha kwamba elimu inawafikia wananchi kiurahisi

“Inabidi sasa kutengenezwe namna ambayo serikali inaweza kutumia vyombo vya mawasiliano kufikisha elimu kuhusiana na ugonjwa huu. Watu wengi wanashindwa kuuelewa kwa sababu ni ugonjwa ambao unaingia taratibu na unachukua kipindi kirefu mpaka mgonjwa anakuja kupata tatizo. Kwa hiyo, wengi wanakuwa hawafahamu ugonjwa huu.” alisema Dkt Ismaili

Kauli mbiu ya siku ya homa ya Ini duniani kwa mwaka 2024 inasema "Ni wakati wa kuchukua hatua. Pima, Chanja, Pata tiba" ikiashiria umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na za makusudi katika kupambana na homa ya ini ili kupunguza athari za ugonjwa huo.

Imetayarishwa na Amri Ramadhani Sauti ya Amerika Dar es Salaam.

Forum

XS
SM
MD
LG