Makundi ya kutetea haki za binadamu yanalilaumu jeshi la Cameroon kwa kuuwa wanavijiji kwenye msako ambao umekuwa ukiendelea mwezi Septemba, wa kuwasaka washukiwa wanaoupinga utawala , madai ambayo yamepingwa vikali na serikali. Jeshi la Cameroon limekiri kwamba wanajeshi wake watatu kutoka kikosi cha wanahewa wiki hii wamewaua wanawake wawili kwenye kijiji kinachotumia lugha ya kiingereza cha Nylbat kilichoko wilaya wa Andeck.
Taarifa iliyotiwa saini na msemaji wa jeshi Serge Cyrill Atongfack inasema kwamba wanajeshi hao walikuwa wametumwa ili kupambana na wanamgambo kwenye eneo la kaskazini magharibi mwa nchi lililokumbwa na matatizo. Ripoti zinasema kwamba walikaidi amri na kuanza kuwamiminia risasi raia wa kawaida, ndipo wanawake hao wawili walipouwawa.