Maandamano ya wananchi kuhusu hali ya hewa yalikusudiwa yafanyika sawa na maadhimisho ya siku 100 za Trump tangu achukue madaraka, kwa mujibu wa waandalizi wa maadamano hayo.
Wanaharakati hao pia wamelaani kile wanachokiona katika uongozi huu ambao hautilii maanani masuala ya mazingira.
Wamesema wanapinga hatua za Trump za kuondoa vikwazo katika uchimbaji wa madini, mafuta na gesi zenye madhara kutoka viwandani katika vinu vinavyozalisha umeme kwa makaa ya mawe, kati ya mambo mengine.
“Sera za uongozi wa Trump ni janga kwa hali ya hewa na jamii kwa jumla, hasa watu wenye vipato vya chini na jamii za watu wa rangi, ambao wako mstari wa mbele wakikabiliwa na migogoro hii,” wamesema wanaharakati wa mazingira, ikiwa ni mkusanyiko wa vikundi 50 vya wanaharakati wa makundi ya kiliberali, katika tamko lao.
Waandamanaji hao walitembea kutoka Bunge la Marekani mpaka ikulu ya White House, ambapo walifanya mkutano mkubwa. Takriban maandamano kama hayo 300 au mikutano imefanyika katika miji mikubwa kutoka Seattle mpaka Boston.
Jijini Washington, waandamanaji waliingia katika joto kali wakati limefikia viwango vya nyuzi 90, wakati huko Denver, kulikuwa na thaluji iliyowashukia mamia ya wanaharakati hao ambao walikusanyika kuhamasisha ushirikiano katika kulinda na kutetea mazingira.