Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 26, 2024 Local time: 10:28

Orodha ya waliouwawa Kenya baada ya uchaguzi Agosti 8


Shirika la Amnesty International
Shirika la Amnesty International

Mashirika ya haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights yametoa ripoti kuhusu watu waliosemekana kuuwawa baada ya uchaguzi wa urais Agosti 8 nchini Kenya. Hii ni orodha kamili kulingana na mashirika hayo:

1. Francis Njuguna, miaka 31

Aliuwawa kwa kupigwa risasi katika kitongoji cha Kariobangi, Nairobi, Agosti 11. Mwili wake ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti Jijini Nairobi.

2. Vincent Omondi Okebe, miaka 27

Alipigwa risasi Agosti 11 katika kitongoji cha Dandora wakati wa maandamano yaliyoandaliwa na wafuasi wa Muungano wa upinzani wa Nasa. Baada ya muda alifariki kutokana na majeraha akiwa Hospitali ya Kenyatta.

3. Thomas Odhiambo Okul, miaka 26

Alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi na polisi Agosti 11 akiwa nyumbani kwake katika kitongoji cha Dandora, Nairobi.

4. Kevin Oteino, miaka 23

Alikufa akiwa njiani anapelekwa hospitali baada ya kupigwa risasi na polisi nje ya geti la nyumba yake katika kitongoji cha Dandora, Nairobi, Agosti 12.

5. Vitalis Otieno, miaka 23

Alikufa akiwa nyumbani kwake kutokana na mshtuko katika kitongoji cha Dandora, Nairobi, Agosti 12. Alipata mshituko huo baada ya kujikuta akiwa katikati ya vurugu iliyokuwa ikiendelea kati ya polisi na wafuasi wa Nasa.

6. Sammy Amira Loka, miaka 45

Alipigwa na bomu la machozi ambapo alivuta gesi ya bomu hilo katika eneo la Kawangware Stage Two, Jijini Nairobi. Alifariki akiwa Hospitali ya Kenyatta Agosti 9.

7. Lillian Khavere, miaka 40

Alikuwa ana ujauzito wa miezi 8 alipopoteza uhai wake. Alianguka baada ya polisi kurusha bomu la machozi na kukanyagwa na kundi la watu lililokuwa linakimbia huko eneo la Kawangware Namba 56 Agosti 9.

8. Festo Kevogo, miaka 33

Alipigwa risasi kichwani na polisi Agosti 9 akiwa Kawangware Namba 56, Nairobi. Alifariki akiwa njiani anapelekwa hospitali.

9. Melvin Mboka Mwangitsi, miaka 19

Aliuwawa kwa kupigwa risasi na polisi katika eneo la Satellite/ Kawangware, Nairobi. Mwili wa marehemu ulikutwa katika chumba cha maiti Hospitali ya Kenyatta.

10. Paul Mungai, miaka 33

Alipigwa risasi ya tumboni. Alikufa kutokana na kuvuja damu ndani ya tumbo akiwa Hospitali ya Kenyatta Agosti 20. Alikuwa mkazi wa Kawangware Namba 56 Nairobi.

11. Zebedeo Mukhala, miaka 42

Alipigwa risasi mguuni na kuanguka chini na kundi kubwa la watu waliokuwa wakikimbia polisi kumkanyaga Agosti 12. Mukhala alifariki August 14 akiwa amelazwa Hospitali ya Mbagathi akipokea matibabu.

12. Violet Khagai, miaka 43

Ni mkazi wa eneo la Kawangware Stage Two. Alipigwa na bomu la machozi na kuvuta hewa yenye pilipili Agosti 12. Alifariki akiwa njiani anapelekwa hospitali.

13. Erick Kwama, miaka 30

Alifariki akiwa Hospitali ya Kenyatta baada ya kupigwa na bomu la machozi lilokuwa limepigwa karibu na alipokuwa, na kuvuta hewa yenye pilipili Agosti 10.

14. Nelvin Amakove, miaka 30

Mnamo Agosti 11, alijikuta katikati ya vurugu za maandamano. Alipigwa risasi mgogoni akiwa anakimbia kutoka katika eneo la Kawangware No 56, Nairobi ambalo polisi walikuwepo. Alifariki papo hapo na mwili wake ulipatikana katika Hospitali ya Kenyatta.

15. Suleiman Khatibu, miaka 25

Raia wa Tanzania ambaye alikuwa mfanyakazi wa mgahawa wa San Valencia katika eneo la Karen. Agosti 11, alipigwa na bomu la machozi kifuani akiwa karibu na polisi. Alitokwa na damu puani, mdomoni na kuaga dunia alipofikishwa Hospitali ya Kenyatta Agosti 18. Alikuwa anaishi eneo la Kinyanjui, karibu na Kawangware, Nairobi.

16. Jeremiah Maranga, miaka 50

Alikuwa ameajiriwa na kampuni ya G4S. Alipigwa na polisi na kuachwa amekufa Agosti 11 huko Kawangware No 56 Jijini Nairobi. Mwili wake wote ulikuwa umetapakaa damu. Alikufa kutokana na kuvuja damu ndani ya mwili na kuharibika kwa kiungo cha ndani ya mwili wakati akisubiri kupata matibabu Hospitali ya Kenyatta.

17. Benson Wandera, miaka 47

Alipigwa risasi na polisi eneo la Kinyanjui, karibu na Kawangware, Nairobi, Agosti 11. Alizikwa huko Busia, magharibi ya Kenya.

18. Silas Owiti Lebo, miaka 18

Alikuwa amepigwa na polisi Agosti 12 katika kitongoji cha Mathare eneo la 4a-C, Nairobi. Alifariki wakati anapokelewa hospitali ili kupatiwa matibabu.

19. Bernard Okoth Odoyo, miaka 25

Alifariki papo hapo baada ya kupigwa risasi mgongoni akiwa mtaa Namba 10 Agosti 9. Alikuwa ni mkazi wa Mathare 4A, Nairobi.

20. Victor Okoth Odoyo, miaka 25

Alikufa papo hapo akiwa eneo Namba 10 baada ya kupigwa risasi mgongoni Agosti 9. Alikuwa anaishi eneo la Mathare 4A, Nairobi.

21. William Waka, miaka 42

Alipigwa risasi kifuani Agosti 9 na mwili wake uliweza kupatikana kwenye chumba cha maiti cha Jiji la Nairobi. Yeye ni mkazi wa Mathare Kaskazini, Nairobi.

22. Boniface Ochieng Owino, miaka 31

Alipigwa risasi katika kifua akiwa eneo la Bondeni huko Mathare, Nairobi, Agosti 12 na kufa papo hapo.

23. David Owino, miaka 28

Alikufa papo hapo kwenye eneo la barabara ya Juja baada ya kupigwa risasi kifuani Agosti 12. Alikuwa anaishi Matharu eneo la Bondeni, Nairobi.

24. Stephanie Moraa Nyarangi, miaka 9

Alizungumziwa katika vichwa vya habari baada ya kupigwa risasi kifuani wakatiakicheza katika varanda ya nyumba yao huko Mathare Kaskazini, Nairobi, Agosti 12.

25. Christopher Samwel Mutua, miaka 32

Ni mhanga mwengine kutoka eneo la Mathare Kaskazini, Nairobi, ambaye alipigwa risasi kufuani akiwa karibu na polisi Agosti 13. Alikufa hapohapo karibu na nyumbani kwake.

26. Fanuel Muruka Amule, miaka 30

Alipigwa risasi Agosti 12 Mathare Kaskazini, Nairobi. Mwili wake ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi maiti Jijini.

27. Raphael Ayieko, miaka 17

Alikufa hapohapo baada ya kupigwa risasi mgongoni katika huko Babadogo, eneo la Kasabuni, Nairobi, Agosti 12.

28. Privel Ochieng Ameso, miaka 18

Alikufa papo hapo baada ya kupigwa risasi kwenye shingo na paja akiwa amepiga magoti Agosti 12. Alikuwa anatokea Babadogo, eneo la Kasabuni, Nairobi.

29. Shaddy Omondi Juma, miaka 17

Alikufa kwa kupigwa risasi akiwa amepiga magoti huko Babadogo, eneo la Kasabuni, Agosti 12. Mwili wake ulipatikana katika jumba la kuhifadhi maiti Jijini likiwa na majeraha 5 ya risasi.

30. Geoffrey Onacha, miaka 34

Aliuawa kwa kupigwa risasi eneo la Kibera, Nairobi, Agosti 10. Mwili wake ulipatikana katika nyumba ya kuhifadhi maiti Jijini.

31. Sharon Imenza, miaka 10

Ni mtoto wa kike wa Geoffrey Onacha (hapo juu). Mnamo Agosti 11, aliaguka na kuzimia na kuaga dunia baada ya kuuona mwili wa baba yake huko Kibera.

32. Henry Onyango Matete, umri wake haujulikani

Alipigwa na polisi Agosti 12 huko Kibera, eneo la Olympic, Nairobi. Alifariki siku moja baadae akiwa amelazwa hospitali ya Muthaiga.

33. Michael Owino, miaka 28

Alipigwa risasi katika eneo la KIbera Olympic Jijini Nairobi. Mwili wake ulitiwa katika mfuko na kuchukuliwa kupelekwa kusikojulikana Agosti 12.

XS
SM
MD
LG