Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Oktoba 10, 2024 Local time: 21:12

Walioshuhudia mauaji ya kimbari DRC wafunguka


Watoto wawili wa kiume wakihamisha samani kutoka shule iliyokuwa ikitumiwa na kundi la waasi la M23 kama kituo cha kijeshi huko Kishishe DRC, tarehe 5 Aprili. Picha na ALEXIS HUGUET / AFP.
Watoto wawili wa kiume wakihamisha samani kutoka shule iliyokuwa ikitumiwa na kundi la waasi la M23 kama kituo cha kijeshi huko Kishishe DRC, tarehe 5 Aprili. Picha na ALEXIS HUGUET / AFP.

Michel alijificha kwenye choo cha nje cha kanisa lake huko Kishishe, katika mji ulioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akisali kuwa waasi wa M23 wasimpate.

Siku hiyo ya Novemba 29, waasi waliuvamia mji uliokuwa na maelfu ya watu na kufanya mauaji yao mabaya sana ambayo hayajawahi kurekodiwa tangu waanzishe kampeni yao mwishoni mwa mwaka 2021.

Zaidi ya raia 170 waliuawa, kulingana na Umoja wa Mataifa.

"Waliwaambia wakae kwenye ukingo wa shimo, na wakaanza kuwapiga risasi," alisema Michel, ambaye alishuhudia mauaji hayo akiwa mafichoni.

Waasi wa M23 waliuteka mji wa Kishishe wiki moja kabla, lakini walirudi tena katika mji huo asubuhi hiyo wakiwatafuta wanamgambo wa Mai-Mai ambao waliwashambulia na kisha kujificha ndani ya nyumba, kulingana na wakaazi kadhaa wa eneo hilo.

M23 -- ambayo inadaiwa kuungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda – kundi hilo limeteka maeneo mengi katika jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Congo na kusonga mbele kwenda maeneo ya ndani kilomita kadhaa kutoka Goma, mji mkuu wa jimbo hilo.

Zaidi ya watu 900,000 walikimbia eneo hilo kabla kundi hilo kufikia, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji limesema.

Kundi la wanamgambo linaloongozwa na Watutsi limeshikilia eneo lote la Kivu Kaskazini kimkakati, ikiwa pamoja na vituo vya mpakani vyenye faida na udhibiti wa barabara nyingi zinazoelekea Goma.

Lakini sababu nyingine zilizowafanya wavutiwe na kuuteka mji wa Kishishe ni kuwa -- mji huo kwa muda mrefu umekuwa ngome ya wanamgambo wa FDLR – ambao wana asili ya kundi la kabila la Wahutu kutoka Rwanda wenye itikadi kali waliotekeleza mauaji ya kimbari kwa Watutsi mwaka 1994 nchini Rwanda.

M23 hivi karibuni walijiondoa katika kijiji hicho cha Kishishe.

AFP iliutembelea mji huo Aprili 5. Majina yote ya watu waliohojiwa yamebadilishwa ili kulinda usalama wao.

Kiongozi wa kijiji aliliambia shirika la habari la AFP kwamba vifo vya watu 120 vilitokea kati ya tarehe 22 na 29 mwezi Novemba, na aliandika kwa mkono orodha ya majina ya watu kwenye kurasa tatu zilizokuwa mfukoni mwake.

Chanzo cha habari hii ni Shirika la habari la AFP

XS
SM
MD
LG