Umoja wa mataifa umesema watu waliokuwa na silaha wamewauwa walinda amani watatu wa UN katika kambi ya wakimbizi kwenye eneo lenye mzozo la Darfur.
Ujumbe wa UN huko Darfur umesema wanajeshi wawili na mshauri wa polisi walikufa katika shambulizi hilo lililotokea jumatatu takriban kilomita 10 kusini mwa EL Fasher kaskazini mwa Darfur.
Walinda amani wengine sita walijeruhiwa na mmoja wa watu hao waliokuwa na silaha aliuwawa.
Mkuu wa ujumbe wa UN katika jimbo la Darfur Ibrahim Gambari alilaani shambulizi hilo. Amesema walinda amani wanafanyakazi kurejesha amani katika kambi ya wakimbizi waliokoseshwa makazi ya Zam Zam ambako shambulizi lilitokea.
Gambari pia alitoa mwito kwa maafisa wa usalama wa Sudan kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
Umoja wa mataifa imesema walinda amani 33 wameuwawa katika ghasia tangu ujumbe wa UN kupelekwa Darfur mwaka 2007.