Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Januari 30, 2023 Local time: 20:41

Walimu Zimbabwe wakataa nyongeza ya mshahara ya asilimia 100, serikali yatishia kuwafuta kazi


Muungano wa waalimu nchini Zimbabwe umekataa nyongeza ya mshahara ya asilimia 100.

Nyongeza hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali kutaka walimu warudi kazini.

Walimu wanasema kwamba mshahara wa dola 180 ni mdogo sana ikilinganishwa na kiwango cha umaskini nchini humo ambacho kimefikia dola 540.

Wanafunzi nchini Zimbabwe wanakwenda shule kila siku, lakini hakuna masomo yanaendelea kutokana na mgomo wa walimu wanaotaka nyongeza ya mshahara.

Shule zilifungwa nchini Zimbabwe mnamo mwezi Machi kufuatia janga la virusi vya Corona.

Serikali ya Zimbabwe imetangaza kuwapa walimu mshahara wa dola 180 mkwa mwezi lakini muungano wa waalimu umekataa nyongeza hiyo.

Tkavafira Zhou, ni rais wa muungano wa waalimu nchini Zimbabwe.

“Kile wafanyakazi wanataka ni mishahara inayolingana na hali ya uchumi ilivyo sasa. Wanataka kulipwa kati ya dola 520 na 550 kwa mwezi. Mshahara wanaopata walimu sasa hata hauwezi kuwasaidia kuelimisha Watoto wao wenyewe na kutekeleza majikumu yao nyumbani.”

Waziri wa elimu ya juu wa Zimbabwe Amon Murwira anasema kwamba kiwango kipya cha mshahara ndicho kile serikali inaweza kulipa kwa sasa na ana matumaini kwamba walimu watakubali na kurudi kazini.

"Serikali inazingatia sana maslahi ya walimu na raia wote wa Zimbabwe wakiwemo wanafunzi. Kwa sasa, walimu wanapewa asilimia 10 ya kufanya kazi katika mazingira magumu na tunatarajia kwamba hatua ambazo serikali inachukua zitasaidia sana katika kuboresha maisha ya wafanyakazi wake. Tunatarajia kwamba walimu watawajibika na kurudi kazini kwa ajili ya wanafunzi ambao hatuwezi kuwatumia kama mtego kutimiza mahitaji yetu.”

Munyaradzi Masiyiwa ni mwalimu wa sayansi katika shule ya upili. Ana umri wa miaka 33. Anasema kwamba anapata pesa nyingi akiuza fagio kwa watu barabarani ikilinganiswa na kufundisha.

“Siwezi hata kununua chakula cha kutosha kulisha familia yangu kwa kutegemea mshahara. Hatua ya serikali ni kejeli kwa walimu. Tunaomba serikali kuangazia swala hili kwa uzito unaostahili sasa hivi, sio kesho. Kama kweli tuna serikali ya watu wa Zambabwe, inastahili kuchukua hatua.” Amesema Masiyiwa.

Kando na kutaka kulipwa mshahara wa dola 500 kila mwezi, walimu wanataka vifaa vya kutosha kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona ndipo warudi darasani.

Serikali inasema kwamba imenunua vifaa hivyo vinavyogharimu dola milioni 6 kwa ajili ya shule.

Serikali hata hivyo imetishia kuwafuta kazi walimu wanaokataa kurudi kazini.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG