Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 20, 2024 Local time: 15:31

Wakongwe wa vuguvugu la MauMau lililopigania uhuru wa Kenya, wamshtaki mahakamani Makamu rais William Ruto.


Makamu rais wa Kenya na mgombea urais William Ruto, akihutubia wafuasi wake kwenye kampeni katika kitongoji cha Karen, jijini Nairobi , kabla ya uchaguzi ujao. Januari 18, 2022. Picha ya Reuters.
Makamu rais wa Kenya na mgombea urais William Ruto, akihutubia wafuasi wake kwenye kampeni katika kitongoji cha Karen, jijini Nairobi , kabla ya uchaguzi ujao. Januari 18, 2022. Picha ya Reuters.

Wakongwe wa vuguvugu la MauMau lililopigania uhuru nchini Kenya, wamemshtaki Naibu Rais wa Kenya William Ruto katika mahakama kuu jijini Nairobi kwa kile wanachokitaja kuwa ni kuasi majukumu ya unaibu rais nchini humo.

Vuguvugu hilo linataka William Ruto kuondolewa kwenye wadhifa wake kwa kukiuka Kifungu cha 147 cha Katiba ya nchi hiyo kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kama Naibu Rais na msaidizi mkuu wa Rais.

Vuguvugu hilo la wakongwe wa vita nchini Kenya, linadai kuwa Ruto ameachana na majukumu yake ya kikatiba kama msaidizi mkuu wa Rais Uhuru Kenyatta na badala yake kujitungia majukumu ya kibinafsi yasioambatana na wadhifa wake.

Katika nyaraka za kesi hiyo mbele ya mahakama jijini Nairobi, vuguvugu hilo linaeleza kuwa Ruto ambaye ni msaidizi mkuu wa rais ndani ya chama tawala cha Jubilee, ameshindwa kutekeleza majukumu ya afisi ya Naibu Rais chini ya Kifungu cha 147 (1) (2) cha Katiba, “na kukiuka vipengele hivyo vya katiba ni ithibati tosha ya kuondolewa afisini kwa utovu wa nidhamu”, amesema Michael Kirungia, aliyewasilisha kesi hiyo kwa mintarafu ya udharura mahakamani humo.

Kirungia katika mawasilisho hayo, ameiambia mahakama kuwa Ruto amejitenga na utekelezaji wa majukumu hayo na kuanza kujihusisha na kampeni za kujipigia debe kugombea urais katika uchaguzi wa Agosti 9, chini ya chama chake kipya cha United Democratic Alliance, chenye kauli ya “kazi ni kazi”.

Ruto amepuuzilia mbali hatua ya kujiuzulu kutoka serikalini hata wakati ambapo rais Kenyatta amechukua hatua za wazi kumuunga mkono aliyekuwa mpinzani wake wa kisiasa Raila Odinga kumrithi katika uchaguzi wa Agosti 9, anapostaafu.

Ruto amekuwa akilalamika kuwa licha ya kumpigia kampeni za kisiasa Kenyatta nyakati hizo kushinda urais mwaka 2013 na 2017, amemgeuka na kumuunga mkono Odinga aliyeshindana naye, mtu ambaye anataja hakutumia muda wake kumfanyia siasa kuwa rais.

Ripoti hii imeandaliwa na mwandishi wa Sauti ya Amerika mjini Nairobi, Kennedy Wandera.

XS
SM
MD
LG