Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa - UNHCR - linashughulikia wakimbizi wa Sudan 162,500 huko Sudan Kusini na Ethiopia. Idara hiyo inasema inategemea idadi hiyo kuongezeka hadi 235,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka. Imetoa wito wa msaada wa dola millioni 220 kusaidia watu hao. Lakini mpaka sasa imepata kiasi kidogo sana cha fedha hizo.
UNHCR inasema idadi ya wakimbizi Ethiopia inaelekea kutulia, wakati hali huko Sudan Kusini inaharibika kila siku ipitayo. Inasema idadi ya watu wanaokimbia mapigano na njaa Sudan inaendelea kuongezeka.
Katika wiki za hivi karibuni, UNHCR inaripoti kumekuwa na ongezeko kubwa la wimbi jipya la wakimbizi wakifika katika jimbo la Upper Nile la Sudan. Na watu wanazidi kuingia humo kwa kasi ya watu 1,000 kila siku.
Msemaji wa UNHCR Adrian Edwards anasema wengi wa wakimbizi hao wako katika hali mbaya wanapofika. Anasema idadi ya watu wanaokufa katika kambi za wakimbizi kutokana na matatizo yao inazidi kuongezeka.