Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 08:52

Waziri wa Kenya Waiguru ajiuzulu


Waziri wa Kenya Ann Waiguru
Waziri wa Kenya Ann Waiguru

Na BMJ Muriithi

Waziri wa ugatuzi nchini Kenya Anne Waiguru amejiuzulu. Bi Waiguru amesema amechukua hatua hiyo kufuatia ushauri kutoka kwa daktari wake kwa sababu ya kile alichokiita “kuathirika kwa afya yangu kutokana na shinikizo kutoka kila pembe.”

Waiguru aliwasilisha barua ya kujiuzulu kwa rais Uhuru Kenyatta siku ya Jumamosi kabla ya kutoa taarifa kwa wanahabari mjini Nairobi.

Bi Waiguru amesema familia yake imeathiriwa mno na kile alichokiita “ushambulizi kutoka kwa watu ambao walitaka niondoke kutoka kwa wizara hii” na kuongeza kwamba masaibu yake yalianza kumkumba alipopuliza kipenga dhidi ya uporaji wa pesa za uma katika wizara hiyo.

Rais Kenyatta wa Kenya
Rais Kenyatta wa Kenya

Hata hivyo, akiwahutubia waandishi wa habari mjini Nairobi, Waiguru alisema yuko tayari kuchukua wadhifa mwingine iwapo atapewa.

“Iwapo rais Kenyatta ataona ni vizuri kunipa kazi nyingine nyepesi, basi nitaifanya,” alisema, huku akionekana kufungia machozi.

Waziri huyo wa zamani amekuwa akikabiliwa na shutuma za usimamizi mbaya wa fedha kwenye wizara yake baada ya kukiri kwamba zaidi ya milioni mia saba zilipotea katika idara ya National Youth Searvice na idara zingine zilizo chini ya wizara hiyo ya ugatuzi na mipango.

Kwa muda wa miezi kadhaa Wakenya wengi wamekuwa wakijadili kama ni haki kwa bi Waiguru kuendelea kusimamia wizara hiyo wakati rais Kenyattaakikabiliwa na shinikizo za kumchukulia hatua kama alivyofanya kwa mawaziri wengine katika serikali yake.

Baadhi ya watu walitaka Waiguru asimamishwe kazi hili uchunguzi dhidi ya shutuma za ufisadi zifanyike.

Baada ya habari kuhusu kuzjiuzulu kwake kuibuka, Wakenya wengi wameendelea kutoa maoni yao hususan kwenye mitandao ya kijamii. Bw Moses Wetangula, ambaye ni mmoja wa Viongozi wa upinzani nchini humo, alisema kwenye mtandao maarufu wa Twitter kwamba Waiguru amejiuzulu “baada ya kumletea uchungu na aibu kubwa rais Uhuru Kenyatta.”

Waziri Waiguru amekuwa akikabiliwa na shutuma za rushwa kwa muda mrefu na baadhi ya wakenya wakiwemo viongozi wa upinzani wamekuwa wakimtaka ajiuzulu. Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akimwunga mkono muda wote licha ya shutuma hizo.

XS
SM
MD
LG