Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 06:50

Wahome aachiliwa kwa dhamana Kenya


Dereva wa mbio za magari nchini Kenya, Maxine Wahome (kushoto) akitoka kizimbani katika mahakama ya hakimu mkazi mjini Nairobi tarehe 12 Januari 2023. Picha na Tony KARUMBA/AFP.

Mahakama ya Kenya siku ya Alhamisi imemuachilia kwa dhamana dereva wa mashindano ya magari nchini humo Wahome Maxine, ambaye amekuwa chini ya ulinzi wa polisi kwa tuhuma za mauaji.

Wahome, mwenye umri wa miaka 27, anadaiwa kumshambulia mpenzi wake na dereva mwenzake Asad Khan aliyekuwa na umri wa miaka 50 katika nyumba yao iliyoko katika mji mkuu wa Nairobi Desemba mwaka jana.

Khan alifariki dunia kutokana na majeraha kwenye kifundo cha mguu wake wa kulia baada ya kukaa hospitali kwa wiki moja.

"Ninampa mtuhumiwa bondi ya shilingi milioni mbili za Kenya, na mdhamini wa kiwango kama hicho cha pesa," hakimu wa mahakama kuu Lilian Mutende alitoa maamuzi hayo, na kuongeza kuwa upande wa mwendesha mashtaka haukuwasilisha ushahidi wa kutosha ili mtuhumiwa anyimwe dhamana.

Mutende alimuamuru Wahome akabidhi hati yake ya kusafiria katika mahakama na akae mbali na mashahidi wote.

Wahome, ambaye alijipatia umaarufu kwa kuwa mwanamke wa kwanza Mkenya kushinda mbio za magari daraja la tatu za WRC Safari Rally mwezi Juni mwaka jana, Wahome alikana makosa.

Mwezi huu aliondolewa kwenye programu ya WRC Young Rally Stars.

Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la AFP

XS
SM
MD
LG