Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Juni 20, 2024 Local time: 20:42

Mgomo wa Wahadhiri na Kudorora Kwa Sekta ya Elimu Kenya


Rais Uhuru Kenyatta
Rais Uhuru Kenyatta

Wahadhiri wa vyuo vikuu wameshiriki maandamano Jumanne kuishinikiza serikali ya Rais Uhuru Kenyatta kutekeleza mkataba wa 2013/17.

Wamesema kuwa kinyume cha hivyo sekta ya elimu itaendelea kuathirika na kurudi nyuma.

Maadamano hayo yamejumuisha muungano wa vyama vya wafanyakazi vyuo vikuu vya Kenya (KUSU) na muungano wa wahadhiri wa vyuo vikuu (UASU).

Wakati mgomo wa Madaktari nchini Kenya ukiingia siku ya 72, bila kuwapo ishara za kupatikana suluhu ya kudumu, mgomo wa wahadhiri wa vyuo vikuu umesababisha shughuli zote za masomo kusimama.

Mapema wiki hii viongozi saba wa chama cha madaktari walihukumiwa kutumikia kifungo cha mwezi moja kwa kupuuza amri ya mahakama iliyowataka kusitisha mgomo wao.

UASU imekuwa ikiitaka serikali ifanye mazungumzo nao licha ya kutoa nyongeza ya asilimia tatu, wakilalamika ongezeko hilo ni dogo mno.

Mwanzoni mwa mwaka huu wahadhiri wa vyuo vikuu nchini waliipa serikali siku saba kutekeleza mkataba wa makubaliano wa mwaka elfu 2013/17 kuhusu kuboresha maslahi yao, lakini wamedai serikali haijaonesha ishara ya kulisimamia suala hilo ipasavyo.

Wahadhiri wameandamana Jumanne kuelekea ofisi za Bunge la Kitaifa kuwasilisha maombi yao ya kutaka kati ya mambo mengine kupewa nyongeza yao ya mshahara.

Walionekana wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe “A professor earns peanuts yet the most educated” yenye maana; profesa analipwa pesa ndogo mno ingawa ni mwenye kuelimika zaidi.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa wahadhiri wanadai kuwa maandamano haya ni sehemu ya kuishinikiza serikali kufanya mazungumzo nao ili kutafuta suluhu juu ya tatizo hilo sugu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Richard Bosire amesema kuwa msimamo wao uko pale pale kwamba mgomo wao utaendelea hadi serikali itapojali maslahi yao.

“Iwapo serikali haitoitisha mkutano wa dharura kufanya mazungumzo nasi, mgomo huu utakuwa wa kupigiwa mfano katika taifa ambalo linaonekana kujivuta kusuluhisha maslahi ya wafanyakazi wake,” amesema mhadhiri huyo.

Aidha, Bosire anailaumu serikali kuu kwa kushindwa kupambana na ufisadi ambao anadai kuwa imeifilisi nchi kwa kiasi kikubwa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya

XS
SM
MD
LG