Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 07, 2024 Local time: 11:43

WAGNER yashambuliwa Libya


Mkuu wa kikundi cha wanamgambo wa Russia Wagner, Yevgeny Prigozhin akiwa kwenye paa la jengo la eneo lisilojulikana, tarehe 24 Juni 2023. Picha na @concordgroup_official / AFP
Mkuu wa kikundi cha wanamgambo wa Russia Wagner, Yevgeny Prigozhin akiwa kwenye paa la jengo la eneo lisilojulikana, tarehe 24 Juni 2023. Picha na @concordgroup_official / AFP

Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani Ijumaa asubuhi yaliipiga kambi ya jeshi la anga iliyoko mashariki mwa Libya, kambi ambayo inatumiwa na mamluki wa kundi la Wagner la Russia. Katika shambulio hilo hakuna madhara yoyote yaliyotokea, afisa mmoja wa jeshi aliliambia shirika la habari la AFP.

Afisa huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema chanzo cha mashambulizi hayo ya usiku kucha katika kambi ya jeshi la anga la Al-Kharruba, iliopo takriban kilomita 150 kusini magharibi mwa Benghazi, "hakijulikani".

Kambi iliyoshambuliwa ni "ile iliyokuwa na wanamgambo wa kundi la Wagner", afisa huyo alisema, akiongeza "hakuna walioathirika".

Libya imekuwa katika mzozo kwa zaidi ya muongo mmoja tangu uasi wa mwaka 2011 uliomng'oa madarakani kiongozi mwenye nguvu Moamer Kadhafi, uasi ambao uliyahusisha mataifa mengine ya kigeni.

Nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imegwanyika kati ya serikali ya mpito ya Tripoli iliyopo upande wa magharibi, na serikali nyingine iliyopo mashariki inayoungwa mkono na mwanajeshi mwenye nguvu Khalifa Haftar.

Pamoja na wapiganaji kutoka Chad, Sudan, Niger na Syria walioajiriwa kama mamluki, kundi la Wagner liko huko kutoa msaada kwa Haftar ikiwa ni pamoja na jaribio lake la hapo awali lililofeli la kuuteka mji mkuu wa Libya.

Mamluki wa Wagner wanaendelea kufanya kazi katika eneo lenye utajiri wa mafuta lililopo mashariki mwa Libya pamoja na eneo lililopo kusini mwa nchi hiyo, ingawa baadhi yao waliondoka kwenda kupigana nchini Mali na Ukraine, wakiunga mkono uvamizi wa jeshi la Russia.

Chanzo cha habari hii ni mashirika ya habari ya AFP

Forum

XS
SM
MD
LG