Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 09, 2024 Local time: 01:26

Wafungwa wajaribu kutoroka kutoka gereza kuu la Kinshasa, DRC


Sehemu ya mji wa Kinshasa, DRC
Sehemu ya mji wa Kinshasa, DRC

Wafungwa walijaribu kutoroka usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu kutoka gereza kubwa zaidi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lililopo Kinshasa, serikali imesema huku ikilalamika juu ya "vifo vya watu."

"Hili ni jaribio la kutoroka katika gereza kuu la Makala. Huduma za usalama zipo eneo hilo kurejesha utulivu na usalama," alisema msemaji wa serikali Patrick Muyaya Jumatatu asubuhi kupitia mtandao wa kijamii X, bila kutoa maelezo zaidi juu ya hali hiyo.

"Hali iko chini ya udhibiti," aliongeza Bwana Muyaya kwenye televisheni ya taifa ya Kongo akiwa Beijing, ambako ni sehemu ya ujumbe rasmi unaoandamana na Rais Félix Tshisekedi kwenye mkutano wa Afrika na China.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Jacquemain Shabani, alilalamikia "vifo vya watu, majeruhi na hasa uharibifu wa mali," katika taarifa ya video iliyotumwa kwa vyombo vya habari. Hata hivyo, hakuna taarifa ya idadi kamili iliyotolewa.

Jumatatu, barabara zinazoelekea gereza la Makala zilikuwa zimefungwa na polisi, waandishi wa habari wa AFP walibaini.

Daddi Soso, fundi umeme mwenye umri wa miaka arobaini anayeishi katika mtaa huo, aliambia AFP kwamba aliamshwa usiku wa manane na milio ya risasi.

"Palikuwa na milio ya risasi kuanzia saa 7:00 au 8:00 usiku, na ikaendelea hadi karibu saa 11:00 asubuhi," alisimulia, akiwa na wasiwasi.

"Palikuwa na vifo na kuna watu walitoroka," aliongeza akidai kuwa aliona magari ya vikosi vya usalama yakibeba miili.

Mamlaka hazijatoa taarifa zozote kuhusu wafungwa walioweza kutoroka.

"Uchunguzi unaendelea ili kubaini na kuwachukulia hatua kali wale waliopanga vitendo hivi vya hujuma," alieleza Waziri wa Sheria Constant Mutamba kupitia X, akitangaza kusitishwa kwa uhamisho wa wafungwa kwenda kituo cha gereza hadi itakapoamriwa vinginevyo.

Gereza la Makala, lenye uwezo wa kuhifadhi watu 1,500 lakini likiwa na msongamano mkubwa, lina wafungwa kati ya 14,000 na 15,000, kulingana na takwimu rasmi.

Mwaka 2017, shambulio la usiku lililofanywa na wanaume wenye silaha lilipelekea wafungwa zaidi ya 4,000 kutoroka.

Forum

XS
SM
MD
LG