Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Septemba 17, 2024 Local time: 22:43

Wafanyabiashara wa Kariakoo wagoma kwa kufunga maduka


Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wakiwa wamebeba mabango walipokuwa wakieleza masikitiko yao juu ya madai ya kuwepo mrundikano wa kodi na rushwa.
Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo wakiwa wamebeba mabango walipokuwa wakieleza masikitiko yao juu ya madai ya kuwepo mrundikano wa kodi na rushwa.

Wafanyabiashara katika soko la kariakoo nchini Tanzania wamefanya mgomo na kufunga maduka wakipinga mrundikano wa kodi.

Wakizungumza na Sauti ya Amerika, Baadhi ya wafanyabiashara wamesema moja ya sababu ya mgomo huo ni hatua Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA kuwalazimisha wafanyabiashara wadogo kutumia mashine za EFD kutoa risiti ambazo zina gharama kubwa za uendeshaji na kuathiri biashara.

Ikiwa si mara ya kwanza kwa wakazi wa Dar es Salaam kushuhudia mgomo wa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo. Mmoja wa wafanyabiashara hao Beatrice John ameiambia sauti ya Amerika, “Mimi nilikuwa ni machinga nilikuwa nanauza bidhaa zangu chini lakini machinga tulifukuzwa barabarani nikaamua kuchukua mkopo nikafungua biashara yangu hii,”

“Ndio nimeanza lakini kila siku TRA wapo hapa wananiambia ninunue mashine nikaenda kuuliza bei ya mashine ni karibuni laki sita hiyo laki sita si bora niongezee mtaji jamani kwahiyo imekuwa ni kero na kila siku wanatutishia.” Aliongeza.

Mfanyabiashara mdogo mwingine Husna Ally anasema kuwa hata baada ya kununua hizo mashine zimekuwa hazina ubora na zinahitaji kutengenezwa kila mara na hivyo kuwasababishia hasara.

“Duka kama hili mtaji mdogo tunalazimika kununua mashine kweli jamani na biashara zenyewe zilivyokuwa ngumu mashine laki sita lakini mtu unanunua mashine lakini siku mbili inaharibika unaenda kutengeneza laki mbili na hamsini tena inaharibika, tumechoka” alisema

Sababu nyingine zinazotajwa na wafanyabiashara hao kugoma kwa mara ya pili ni kutokana na serikali kushindwa kutatua kero walizowasilisha katika mgomo wa kwanza ikiwemo mrundikano wa kodi, kuondoshwa kwa kikosi kazi cha ukusanyaji kodi pamoja na kuondoa sheria mpya ya usajili wa stoo.

Ibrahimu Ally amesema changamoto nyingine ni utozwaji wa kodi mara mbili bandarini pamoja na kwenye maduka hali inayopelekea kuwepo kwa mianya ya rushwa na hivyo kuendelea kuwadidimiza wafanyabiashara katika soko hilo.

“Unajua kinachotuletea shida ni kwamba mizigo yote hii inapita bandarini lakini sasa mtu umeshakadiriwa kodi bandarini tayari mzigo kule bandarini umeshalipiwa tayari lakini mtu anakuja anakufuata tena na huku dukani na umeshakadiriwa’ Na kuongeza kuwa “mbona sisi tunasafiri tunaenda nchi nyingine kama China, Dubai hakuna mambo kama haya sasa haya yanatuletea shida na tunatengeneza mianya ya rushwa unajikuta sasa inabidi na TRA nae umpe rushwa sasa maisha gani haya, tunaishi kwa shida.”

Aidha Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alieleza makubaliano yaliyofikiwa katika kikao kazi kati ya viongozi wa wafanyabiashara na serikali na amesema serikali imekubali kusitisha zoezi la ukaguzi wa risiti za kielekroniki (EFD) uliyokuwa ukifanywa na TRA.

“TRA inasitisha operesheni zake maarufu kama kamata kamata mpaka pale itakapokamilisha utaratibu mpya wa kuweka mfumo mzuri zaidi wa kukusanya mapato na hususani katika suala zima la kupatikana kwa nyaraka” alisema

Waziri huyo wa Mipango na Uwekezaji pia alisema kuwa serikali itaendelea kushughulikia changamoto zote za wafanyabiashara zilizoibuliwa wakati wa mkutano wao na Waziri Mkuu na hivyo amewataka wafanyabiashara kuvuta subira.

Forum

XS
SM
MD
LG