Wabunge hao wamezuiliwa nje kidogo ya majengo ya bunge katika mji mkuu Kampala wakati walipokuwa wakijiandaa kuandamana hadi wizara ya mambo ya ndani ambako walikusudia kukabidhi hati ya maandamano kwa waziri.
Walikuwa wakipinga kile walichosema ni ukatili wa polisi na matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa kutawanya shughuli mbalimbali zilizoandaliwa na wabunge wanawake katika majimbo yao katika wiki za hivi karibuni.
“Ilikuwa kama wanawakamata magaidi," naibu spika wa bunge Thomas Tayebwa alisema kupitia mtandao wa Twitter.
"Kukamatwa kwao kulifanywa bila aibu kwenye milango ya Bunge. Kwa hivyo sijui kama kweli tuko salama ikiwa watu wanaweza kuletwa kwenye milango ya bunge ili kuja kuwapiga wananchi”
Video za vurumai hiyo zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha maafisa wa polisi wakijitahidi kuwasukuma ndani ya gari wabunge hao ambao wote walikuwa wamevaa mavazi meusi.
Msemaji wa polisi Luke Owoyesigyire alikanusha kuhusu maafisa hao kutumia nguvu kupita kiasi. Aliwashutumu wabunge hao kwa kukaidi kukamatwa na kuwajeruhi baadhi ya maafisa wa polisi.
Chanzo cha habari hii ni shirika la habari la Reuters