Muungano wa Congo River Alliance ulinukuliwa Jumatatu ukisema kwamba kwamba haukuwa na nia ya kuteka Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, baada ya kuuteka mji mkubwa zaidi wa mashariki mwa Kongo wa Goma wiki iliyopita.
Katika taarifa, muungano huo ulisema: "Tunasisitiza ahadi yetu ya kulinda na kutetea raia."
Mapigano mashariki mwa DRC yamepelekea maelfu ya watu kuhama makazi yao katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Tangu kuanza kwa mwaka 2025, zaidi ya watu 400,000 wamelazimika kuondoka kwenye makazi yao, kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.
Hayo yamejiri katika siku ambayo ofisi ya rais wa Kenya ilitangaza kuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Felix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame walikubali mwaliko kwa mkutano wa pamoja, wa jumiya za Kusini mwa Afrika (SADC) na Afrika Mashariki (EAC), kujadili amani mashariki mwa DRC ambao umepangwa kufanyika Ijumaa na Jumamosi nchini Tanzania.
Rais wa Rwanda Paul Kagame - ambaye pia ni kamanda mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda - alisema hajui kama wanajeshi wa nchi yake walikuwa nchini DR Congo, kwa mujibu wa shirika la habari la CNN.
Rwanda Jumapili ilikubaliana na pendekezo la kufanyika kwa mkutano utakaosimamiwa na SADC na Jumuia ya Afrika Mashariki kujadili mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku Tanzania ikitangaza pia kwamba wanajeshi wake wawili waliuawa katika mapigano ya hivi karibuni.
Waasi wa M23 waliuteka mji wa Goma wiki iliyopita na kutishia kusonga mbele hadi mji mkuu wa Kinshasa.
Jumuia ya nchi za kusini mwa Afrika (SADC) siku ya Ijumaa ilitoa wito wa kufanyika kwa mkutano utakaosimamiwa na SADC na Jumuia ya Afrika Mashariki “kuamua juu ya suluhu la hali ya usalama nchini DRC”.
Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda “imekubaliana na pendekezo hilo” na kuongeza katika taarifa kwamba “imekuwa ikiunga mkono kila mara suluhisho la kisiasa kwa mzozo unaoendelea huko DRC”.
Rais wa Rwanda Paul Kagame hakuhudhuria mkutano wa dharura wa SADC, lakini Rais wa DRC Felix Tshisekedi alihudhuria kwa njia ya mtandao. Rwanda sio mwanachama wa SADC.
Mkutano wa SADC uliitishwa baada ya wanajeshi wa Afrika Kusini na Malawi kuuawa katika mapigano karibu na Goma, ambako walikuwa wanahudumu katika kikosi cha nchi wanachama wa SADC (SAMIDRC). Kikosi hicho kilikuwa na jukumu la kuisaidia DRC kupata amani na usalama wa kudumu.
Jumapili, Tanzania ilitangaza kwamba wanajeshi wake wawili katika kikosi cha SAMIDRC waliuawa pia katika mapigano ya hivi karibuni. Msemaji wa jeshi Gaudentius Ilonda alisema wanajeshi wengine wanne walijeruhiwa na wanapewa matibabu huko Goma.
Wanajeshi 13 wa Afrika Kusini, raia watatu wa Malawi na mmoja wa Uruguay waliokuwa wanahudumu katika kikosi cha MONUSCO na SAMIDRC waliuawa pia katika mapigano ya DRC.
Forum