Radio moja ya kijamii imefungwa kuanzia katikati mwa mwezi Juni, waandishi wake wawili kupigwa vibaya kwa saa kadhaa na waasi hao.
Waliachiliwa huru baada ya kuambiwa kwamba watauawa endapo wataendelea kutoa taarifa kwa jeshi la serikali kuhusu mahali waasi hao walipo na shughuli zao.
Kundi la M23 linawashutumu waandishi wa habari na raia kwa kushirikiana na serikali.
Katika mahojiano na kamati ya kuwalinda waandishi wa habari CPJ, msemaji wa kundi la M23 alikanusha taarifa za waasi hao kuwapiga waandishi wa habari.
Waasi washambulia kituo cha radio, waandishi watishiwa maisha
Kituo cha radio cha Sauti ya Mikeno (RACOM), katika mji wa Bunagana kimefungwa baada ya watu wanaoaminika kuwa waasi wa M23 kubeba mitambo na vifaa vyake mwezi Juni tarehe 13.
Zaidi ya wafanyakazi 20 wa radio RACOM, wamekwenda mafichoni kwa kuhofia maisha yao.
Mwandishi mmoja wa kituo hicho amezungumza na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika, baada ya kuomba kwamba tusitaje jina lake wala kusema mahali alipo kwa kuhofia maisha yake.
Kwa sababu ya uandishi huu, tutamuita Oscar, japo sio jina lake halisi. Amesema kwamba alizuiliwa na waasi wa M23 baada ya kukamatwa akiwahoji wakimbizi katika kambi ya wakimbizi ya Nyakabande, wilayani Kisoro nchini Uganda.
Amesema kwamba baadaye, aliambiwa na wafanyakazi wenzake kwamba mwandishi mwenzake kwenye kituo hicho, Henry Hererimana Serushago, naye alikuwa amekamatwa na waasi hao, kufungwa kamba na kupigwa viboko kwa saa kadhaa kabla ya kuachiliwa huru.
Waandishi hao wawili walisafirishwa na watu tofauti, wakati tofauti, kutoka Nyakabande hadi Bunagana. Waliachiliwa Julai 5. Oscar aliambiwa na waasi hao kwamba “asiendelee kushirikiana na maadui.”
Serushago, katika mahojiano na CPJ, alisema kwamba alifungwa miguu na mikono, kucharazwa viboko na kupigwa mateke kwa saa kadhaa kabla ya kuachiliwa Julai 5.
Oscar na Serushago wamejificha. Waandishi wa habari walio karibu nao wameiambia idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika kwamba wanaishi maisha ya uoga na hawataki mtu yeyote ajue mahali wanakoishi.
Raia wanahofia Maisha yao na kuishi kwa uoga mwingi
Sehemu ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inapakana na Rwanda. Wakaazi wa sehemu hiyo wanaishi kwa uoga mwingi sana.
Wanapokea vitisho vya kuuawa kutoka kwa makundi yenye silaha yanayopigania utajiri mkubwa wa madini.
Dhahabu, almasi na madini mengine yanayotumika kote duniani kutengeneza magari yanayotumia nguvu za umeme, betri na vifaa muhimu katika simu za rununu pamoja na kompyuta, yanapatikana Mashariki mwa DRC.
M23, mojawapo ya makundi ya waasi Mashariki mwa DRC yameongeza mashambulizi katika sehemu hiyo tangu mwishoni mwa mwaka uliopita 2021.
DRC imeishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kulisaidia kundi hilo. Rwanda imepinga madai hayo.
Maandamano kutoka Monusco kuondoka DRC yameongezeka
Mnamo mwezi Juni tarehe 20, viongozi wa jumuiya ya Afrika Mashariki walikutana jijini Nairobi Kenya na kukubaliana kuunda jeshi la pamoja kupambana na makundi ya waasi Mashariki mwa DRC. Viongozi hao vile vile waliyaamrisha makundi hayo kujisalimisha. Hata hivyo, waliyokubaliana hayajatekelezwa na mapigano yanaendelea.
Watu 12 waliuawa Julai 26 kufuatia maandamano ya raia dhidi ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO, mjini Goma na Butembo. Waandamanaji wanadai kwamba jeshi la Umoja wa Mataifa limeshindwa kukabiliana na makundi ya wapiganaji.
Waandamanaji vile vile walikabiliana na polisi wakati walipokuwa wakiandamana kutaka kikosi cha jeshi la Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo, kilomita 24 Magharibi mwa Goma, Julai 27, 2022.
Mwanajeshi mmoja wa Umoja wa Mataifa na afisa wawili wa kikosi hicho waliuawa.
Mwandishi wa VOA ameambiwa atakamatwa Pamoja na jeshi la serikali
Mnamo Julai 13, vyombo vya habari vya Uganda vilimnukuu mkuu wa wilaya ya Kisoro, nchini Uganda, Haji Shafiq Sekandi, akisema kwamba “waasi wa M23 walikuwa wakivuka mpaka na kuingia Uganda kusajili wapiganaji.”
Mwandishi wa Sauti ya Amerika, ambaye ameripoti kuhusu vita vya DRC kwa miaka mingi, ameripoti kupokea simu kutoka kwa watu wanaojitambulisha kuwa wanachama wa kundi la M23, wakimtishia maisha.
Mojawapo ya simu alizopokea, aliyempigia alimwambia kwamba, “una chuki dhidi yetu. Tutakukamata pamoja na hao wanajeshi wa serikali.”
Mwandishi wa VOA amesema kwamba amezungumza na makamanda wa M23 mara kadhaa, walio ndani na nje ya DRC, na kuwaeleza majukumu yake kama mwandishi wa habari, lakini bado anapigiwa simu na kutishiwa maisha.
Kundi la kutetea maslahi ya waandishi wa habari limelaani mashambulizi
Tuver Wundi mratibu wa kundi la waandishi wa habari wanaofanya kazi katika mazingira hatari, amekemea vitendo vya kundi la M23 dhidi ya waandishi wa habari.
“Mwandishi wa habari hahusiki na vita. Anaueleza ulimwengu yanayofanyika katika vita,” Wundi ameiambia idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika. “Hatuelewi kwa nini wanashambulia waandishi wa habari. Waandishi wengi wanaofanya kazi katika sehemu zinazoshikiliwa na waasi wa M23 wametishiwa na wamekwenda mafichono. Waandishi wa radio za kijamii wamejificha. Hawataki kufanya kazi Bunagana. Hawapo huru hata kushika simu wanapopigiwa. Wameamua kuzima simu zao.” Ameendelea kusema Tuver.
Akizungumza na CPJ wiki iliyopita, afisa wa ngazi ya juu wa M23 David Mugave, amesema kwamba shambulizi ya Julai 5 dhidi ya waandishi wa habari “halikutekelezwa na wanachama wa M23 na kwamba hawakuvamia na kuchukua mitambo ya radio RACOM.” Alisema kwamba huenda hayo yote yalitekelezwa na wanachama wa kundi jingine.
Raia wanashambuliwa, kuuawa
Shirika la Human Rights Watch (HRW) limesema kwamba waasi wa M23 wameanza kuwashambulia raia.
Katika ripoti yake ya wiki iliyopita, HRW limesema kwamba waasi wa M23 wameua raia 29, wakiwemo vijana wawili, katikati mwa mwezi Juni. Baadhi ya waliouawa walipigwa risasi walipojaribu kutoroka. Wengine waliuawa kwa kupigwa risasi wakiwa karibu sana na waliowaua.
“Tangu kundi la M23 lilipodhibithi miji na vijiji katika jimbo la Kivu Kaskazini mnamo mwezi Juni, wametekeleza uhalifu mkubwa na wa kutisha dhidi ya raia.” Inasema ripoti ya HRW ambayo vile vile inaorodhesha uhalifu huo na kutaja mahali ulitkookea.
Wanajehi wa Monusco wameuawa, maandamanao yanaendelea
Umoja wa mMtaifa una karibu wanajeshi 12,400 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wanajeshi hao wamekuwa wakiondolewa pole pole katika miaka ya hivi karibuni.
Maandamano ya raia wa DRC kutaka wanajeshi hao waondoke yanaendelea.
Watu wawili waliuawa Julai 31 na 15 kujeruhiwa baada ya wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kufyatua risasi karibu na mpaka na Uganda.
Wanajeshi 5 wa Umoja wa Mataifa – 3 kutoka Morocco na 2 kutoka India – waliuawa wiki iliyopita kutokana na maandamano ya mjini Butembo.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC