Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 07, 2022 Local time: 02:22

Waasi wa M23 wameambia VOA kwamba wanasubiri utekelezaji wa mkataba


Wanajeshi wa DRC wakishika doria karibu na mlima Mbuzi, Rutshuru. wanajeshi hao wanapambana na waasi wa M23. PICHA: AFP

Kundi la waasi wa M23 wanaopigana na wanajeshi wa serikali FARDC, limesema kwamba halitachoka kudai haki ya raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na kutaka makubaliano ya mkataba yaliyofanyika Nairobi kenya kutekelezwa.

Msemaji wa kundi hilo Meja Willy Ngoma, ameambia mwandishi wa idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika VOA, Kennes Bwire kwa njia ya simu kwamba serikali ya rais Felix Tshisekedi imekataa kutekeleza mambo waliyokubaliana alipoingia madarakani, na badala yake kutuma wanajeshi wake kuwashambulia.

Mj. Ngoma amedai kwamba mapigano ya hivi karibuni yanatokana na jeshi la Congo kuanza kile ametaja kama ‘uchokozi’ badala ya kutimiza ahadi.

“Sisi tunajibu mapigo peke yake. Ni hao wamekuja kushambulia ngome zetu. Sisi tunajibu mapigo yao na kuwafukuza mbali kabisa.” Amesema Meja Ngoma.

Mkataba kati ya serikali ya DRC na waasi wa M23

Kundi la M23 lilisaini mkataba na serikali ya Joseph Kabila, mnamo mwezi Desemba 2013.

Hafla ya kusaini makubaliano hayo ilifanyika katika ikulu ya rais ya Nairobi, Kenya, na ilisimamiwa na rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kundi hilo lilianza vita dhidi ya serikali ya Congo April 2012, likishutumu serikali ya Kabila kwa kuwatenga watu kutoka jamii ya Tutsi na kukataa kuheshimu mikataba ya amani iliyokuwa imefikiwa awali.

Mkataba wa Nairobi ulifikiwa baada yakundi hilo kupigwa na wanajeshi wa serikali ya DRC wakisaidiwa na wanajeshi wa umoja wa mataifa.

M23 ni kundi lililoundwa mwaka 2012 baada ya kuishutumu serikali kwa kukosa kuheshimu mkataba wa amani uliosakuwa umesainiwa mwezi March tarehe 23 2009 (M23)

“Tulikubali kusaini mkataba wa Nairobi. Tulisaini tena mkataba wa Kinshasa na rais Felix Tshisekedi alipoingia madarakani baada ya mazungumzo ya miezi 14 na tukakubaliana kuhusu maneno mengi sana. Tunasubiri watekeleze maneno ambayo tulizungumza. Badala yake, wamekuja kushambulia ngome yetu. Sisi tunajibu mapigo yao.” Amesema Meja Ngoma.

Maswala yenye utata

Kulingana na Meja Ngoma, wanataka serikali ya DRC ifanye mazungumzo ya kitaifa kuhusu amani, waasi hao waajiriwe na kuruhusiwa kuhudumu katika jeshi la serikali FARDC, wanasiasa wa kundi hilo washirikishwe kwenye serikali, Jeshi la serikali lipambane na kushinda nguvu kabisa makundi mengine ya waasi kama allied democratic movement ADF.

“Tulimwambia Tshisekedi kwamba tupo tayari kufanya kazi katika jeshi la Congo na kama wamekataa, tupo tayari kurudi vijijini kwa mapigano na kundi la ADF kwa sababu tunaona wanaendelea kuua ndugu zetu.” Ameeleza Ngoma akiongezea kwamba “hatupendi kupigana na serikali ya Congo. Sisi tunataka amani ndio maana tulisitisha mapigano ili tutafute na tujenge amani ndani ya Congo.”

Makundi mengine ya waasi kama Aliied democratic forces, Mai main a Codeco, yamekuwa yakishambulia vijiji na kuuwa raia mashariki mwa Congo.

Ndege ya UN yaangushwa

Mapigano kati ya M23 na jeshi la Congo yalipelekea kuangushwa kwa ndege ya kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa na kuuawa kwa wanajeshi wake 8. Hakuna maelezo zaidi yametolewa kufikia sasa.

Pande zote katika vita hivyo zilishutumiana kwa kuangusha ndege hiyo na hakuna habari kamili imetolewa kufikia sasa.

Msemaji wa kundi hilo anasisitiza kwamba sio waliohusika na kuangusha ndege hiyo na badala yake anasema wao hawawezi kushambulia vikosi vya usalama vinavyolinda raia wa Congo dhidi ya adui, anaodai ni makundi kama ADF, wala M23 haliwezi kushirikiana na makundi hayo.

“Sisi tulikuwa katika jeshi la Congo. Tulikuwa ndani ya serikali. Sisi ni raia wa Congo, tunapenda nchi yetu, tunapenda mabadiliko ndani ya nchi yetu. Hatuwezi kusikilizana na ADF ambao ni adui wa raia wa Congo. Wanaua wakongo, wanaua ndugu zetu, dada, baba na mama wetu wanamaliza. Tunataka tupambane na hao waasi ili turudishe amani ndani ya Congo.”

Je M23 wanapigania nini haswa?

“sisi tunataka amani ya raia wote wa Congo bila ubaguzi wa aina yoyote. Kila raia wa Congo anastahili kuwa huru ndani ya nchi yake. Hatutaki baadhi ya raia wa Congo wawe wa muhimu kuliko wengine. Tunataka makundi yote ya waasi kama ADF yaondoke Congo.” Amesema Meja Willy Ngoma.

Marais Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda), Uhuru Kenyatta (Kenya) na Felix Tshisekedi (DRC) wanaripotiwa kukutana Nairobi April 9 2022 kujadili swala la waasi wa M23 na serikali ya Congo. Hakuna taarifa imetolewa kuhusu mkutano huo kufikia sasa.

Serikali ya DRC imeishutumu Rwanda kwa kuwasaidia wapiganji wa M23, madai ambayo meja Ngoma anakanusha akisema kwamba “kamanda wetu ni Generali Sultan Makenga.”

Mkutano huo unajiri siku chache baada ya waasi wa M23 kutangaza kusitisha vita ili kuruhusu mazungumzo ya amani kufanyika.

“Hiyo ni maneno ya wanasiasa. Mimi ni mwanajeshi. Niko msituni kwa mapambano. Sisi tunapenda amani na tunataka amani irejee nchini mwetu. Hivyo tu.”

Shutuma za DRC dhidi ya Rwanda na Uganda kuwasaidia M23

Serikali ya DRC vile vile imewahi kushutumu Uganda kwa kuwasaidia waasi hao.

Uganda na Rwanda zimesema shutuma hizo hazina msingi wowote.

Karibu waasi 1,500 wa M23, alikuwa wakikaa katika kambi ya mafunzo ya kijeshi ya Bihanga, magharibi mwa Uganda kabla ya kurudi DRC.

“Mimi nilikuwa nakaa katika hiyo kambi ya jeshi katika wilaya ya Ibanda wakati tukidubiri watekeleze mkataba wa Nairobi. Generali wetu aliamua kurudi nchini na sisi wote tukamfuata. Nilikuwa nafungiwa vibaya na serikali ya Uganda. Walikuwa hawataki tumfuate General Sultan Makenga. Niliteswa vibaya sana hadi balozi wa Congo nchini Uganda alikuja gerezani kunijulia hali. Tumekaa milimani miaka 5 bila kuchokoza wanajeshi wa serikali. Ni wao wamekuja kutuchokoza,” Meja Ngoma ameambia idhaa ya Kiswahili ya sauti ya Amerika VOA.

Maelfu ya raia wa DRC wamekuwa wakikimbilia Uganda kutokana na mapigano hayo.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG