Mauaji hayo yanajiri wiki moja baada ya shambulio kama hilo ambalo lillisababisha vifo vya zaidi ya watu 20.
“Kulikuwa na mashambulizi ya wakati mmoja kati ya saa kumi na saa kumi na moja alfajiri kwenye vijiji vitatu,” afisa wa eneo hilo Dieudonne Malangai amesema.
Malangai ameiambia AFP kwamba “waligundua miili 7 katika kijiji cha Manyala, na huko Ofay kulikuwa miili nane, ikiwemo saba ya wanawake.”
Chanzo kutoka mashirika ya misaada kimethibitisha vifo vya watu saba huko Manyala na vingine nane huko Ofay.
“Waasi hao wa ADF walishambulia pia kijiji cha Bandibese lakini walitimka baada ya wanajeshi kuingilia kati na hakuna raia waliouawa katika kijiji hicho,” amesema Malangai baada ya mashambulizi hayo kwenye vijiji vya mkoa wa Ituri unaopakana na Uganda.
Wapiganaji wa ADF walishtumiwa pia kwa mashambulizi ya wiki iliyopita katika mkoa jirani wa Kivu Kaskazini ambayo yalisababisha vifo vya watu 23. Katika mkoa huo huo watu 14 waliuawa katika shambulizi la bomu kwenye kanisa la Kipentekoti.