Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 19, 2025 Local time: 17:34

Waandishi wanazuiliwa Sudan Kusini kwa kuchapisha video ya rais Kiir ‘akijikojolea’


Rais wa Sudan kusini Salva Kiir akishuka ndege Nov. 1, 2017
Rais wa Sudan kusini Salva Kiir akishuka ndege Nov. 1, 2017

Waandishi wa habari sita nchini Sudan Kusini wanazuiliwa na polisi baada ya kudaiwa kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii picha iliyomuonyesha rais wa nchi hiyo Salva Kiir ‘akijikojolea’.

Muungano wa waandishi wa habari nchini Sudan Kusini umethibitisha ripoti za kukamatwa kwa waandishi hao.

Waandishi hao wanafanya kazi na shirika la habari la serikali SSBC.

Video ambayo imekuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii tangu mwezi Desemba inaonyesha kitu kinachoonekana kama mkojo ukitiririka kutoka kwenye nguo za rais Salva Kiir mwenye umri wa miaka 71 wakati wa hafla ya kitaifa, wimbo wa taifa ulipokuwa unacheza.

Rais wa muungano wa waandishi wa habari nchini Sudan Kusini Patrick Oyet, amesema kwamba waandishi hao walianza kukamatwa Jumanne na Jumatano.

Oyet amesema kwamba waandishi hao wanazuliwa kwa sababu maafisa wa serikali wanaamini kwamba “wanajua namna video hiyo ya rais akijikojolea ilivyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.”

Juhudi za kuwafikia maafisa wa serikali kwa taarifa zaidi, akiwemo waziri wa habari Michael Makuei na msemaji wa usalama wa taifa David Kumuri, hazikufanikiwa.

Kiir amekuwa rais wa Sudan Kusini tangu nchi hiyo ipate uhuru mwaka 2011.

Maafisa wa serikali wamefutilia mbali ripoti kwamba rais Kiir ni mgonjwa.

Waandishi waliokamatwa ni pamoja na wapiga picha Joseph Oliver na Mustafa Osman; wahariri wa video Victor Lado; waandishi Jacob Benjamin; Cherbek Ruben na Joval Toombe wanaofanya kazi katika chumba cha kuelekeza matangazo.

XS
SM
MD
LG