Muungano huo wa vyama vya upinzani unaojulikana kama G58 uliungana na chama cha rais wa zamani Alpha Conde RPG, kutangaza nia yao ya kupinga marufuku hiyo na kushtumu “ubabe” wa kiongozi wa kijeshi Kanali Mamady Doumbouya katika taarifa kwa vyombo vya habari.
Katika nchi ambayo imezoea ghasia za kisiasa, vyama hivyo vimeonya kwamba viongozi wa kijeshi “watawajibika pekee yao kwa kuzorotesha” hali ya kijamii katika siku zijazo.
Wakikerwa na ukandamizaji, umaskini na ufisadi chini ya utawala wa Conde, wengi waliukaribisha uongozi wa kijeshi uliponyakua madaraka kutoka kwake mwezi Septemba mwaka jana.
Lakini malalamiko yanaongezeka miongoni mwa vyama vya siasa.
Kundi la G58 na chama cha RPG wamesema katika taarifa yao kwamba hawakubaliani kamwe na marufuku mpya ya maandamano iliyotangazwa siku ya Ijumaa, na wameazimia “kutetea utawala wa sheria”, na katika hali hii kutetea haki ya kuandamana.
Wamesema wataunda kamati ya kuandaa “maandamano ya amani siku zijazo.”