Mzozo wa kisiasa nchini Burundi unaathiri uchumi wa nchi ambao unalega lega. Mashirika ya kimataifa ya misaada yanatishia kujitoa huku ukosefu wa ajira ukiwa unazidi kuongezeka na bei za bidhaa za msingi nazo zikipanda kila siku.
Katika ghala moja la mchele mjini Bujumbura harakati zote zimesimama ghafla wiki chache zilizopita. Polisi walifika na kumshutumu meneja wa ghala hiyo kwa kuwauzia mchele waandamanaji. Mamlaka haraka zimeifunga ghala hiyo alisema mfanyakazi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina kwasababu za kiusalama.
Mfanyakazi huyo ambaye anashughulika kuwapakilia mchele wateja na kawaida hulipwa takriban dola mbili mpaka tano kwa siku alisema hali hivi sasa ni ngumu sana na mwisho wa siku hurejea nyumbani akiwa hana hata senti moja. Alisema kufungwa kwa ghala hiyo kumemuathiri kila mtu, wafanyakazi na wafanyabiashara kama yeye. Kila mtu maisha yake yameathirika.
Katika muda wa wiki chache zilizopita Burundi imekabiliwa na mzozo mkubwa wa kisiasa tangu kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika muda wa muongo mmoja uliopita.
Maandamano ya ghasia yamekuwa yakitokea kila siku katika mji mkuu Bujumbura baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza azma yake ya kuwania awamu ya tatu ya uongozi. Uamuzi ambao wakosoaji wanadai unakiuka katiba ya nchi.
Wiki kadhaa za ghasia zimekuwa na matokeo makubwa kwa uchumi tete wa moja ya nchi ambazo ni maskini sana duniani.
Baadhi ya maduka na makampuni yalilazimika kusimamisha kwa muda shughuli zao za kibiashara kwasababu ya ukosefu wa usalama. Vizuizi barabarani vilizuia usafirishaji wa bidhaa za msingi za chakula kama vile mchele, alisema mchuuzi mmoja katika soko lililopo mjini Bujumbura.