Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 27, 2024 Local time: 02:16

Viongozi wa UAE, Saudi Arabia wakutana baada ya waasi kuiteka Aden


Wapiganaji wa jeshi lililojitenga linalosaidiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu wakiwa mjini Aden baada ya mapambano na vikosi vya serikali Agosti 10, 2019. REUTERS/Fawaz Salman/File Photo
Wapiganaji wa jeshi lililojitenga linalosaidiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu wakiwa mjini Aden baada ya mapambano na vikosi vya serikali Agosti 10, 2019. REUTERS/Fawaz Salman/File Photo

Mwana Mfalme mrithi wa Umoja wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohammed Bin Zayed al Nahyan alikutana na mfalme wa Saudi Arabia, Salman Bin Abdelaziz na mwanawe Mohammad, mjini Mecca kujadili matukio mapya ya kutekwa mji wa Aden, Yemen.

Mazungumzo yamefanyika baada ya wapiganaji wanaotaka kujitenga wa Yemen ya Kusini kuchukuwa udhibiti wa mji mkuu wa kusini wa Aden kutoka serikali inayotambulika kimataifa ya Rais Abdrabbu Mansour mwishoni mwa wiki.

Utulivu warejea Aden

Wakizungumza na shirika la habari la AFP wakazi wa Aden wanasema utulivu umerudi katika mji wao na hali ya maisha imeanza kuwa ya kawaida.
Pia wapiganaji hao wameahidi kuendelea kufanya kazi na muungano unaogozwa na Saudi Arabia .

Pia AFP imeripoti viongozi wa Saudi Arabia wameanza juhudi za mazungumzo baada ya kuonekana muungano unaongozwa na taifa hilo la kifalme kuanza kugawika kuhusiana na hali huko Yemen.

Hii inafuatia kutekwa kwa majengo ya serikali na wapiganaji wanaotaka kujitenga upande wa kusini.

Aidarus al Zubaidi

Kiongozi wa kundi hilo la la Southern Transitional Council STC, Aidarus al Zubaidi amesema ataheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano na yuko tayari kwa mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Saudi Arabia.

Rais wa serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa Abdrabbu Mansour Hadi, alikutana pia na mfalme salman siku ya Jumapili na mtoto wake Muhammed na kukubali kushiriki kwenye mazungumzo hayo.

Kwa muda wa miaka mitano mapigano nchini Yemen yameendelea kati ya Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran na wafuasi wa serikali inayoungwa mkono na mungano wa nchi za Kiarabu unaongozwa na Saudi Arabia.

Lakini tangu Alhamisi wiki iliyopita mapigano yalizuka kati ya makundi ya kisunni yanayoungwa mkono na mungano wa nchi za kiarabu. Kufuatana na Umoja wa Mataifa karibu watu 40 wameuliwa na 260 kujeruhiwa tangu kuanza mapigano ya Aden.

Mfanyakazi wa benki

Abdulrahman Bakkar mfanyakazi wa benki anasema anashukuru hali imetulia.

Abdulrahman mfanyakazi wa benki mjini Aden amesema : "Hali ni tulivu. Naomba mwenyezi mungu awalinde ndugu zetu wa kusini ambao wamechukuwa udhibiti kamili wa mji. Amani imerudi na watu wanarudi kazini.

Kulingana na UN, Yemen iko katika janga kubwa ka kibinadamu kutokana na mgogoro unaoendelea ukikadiria kwamba asilimia 80 ya wakazi milioni 24 wa taifa hilo wanahitaji msaada wa dharura.

Kituo cha ukaguzi

Imad al din Ahmad, mkuu wa kituo cha ukaguzi cha Khor Maksar anafurahi hali imetulia huko kusini kwa sasa.

Amesema : "Kila kitu kiko sawa Aden. Kila kitu kimerudi kuwa cha kawaida na hata bora zaidi. Kama unavyoshuhudia usafiri unaendelea vyema watu wakirudi sokoni. Tunawashukuru viongozi wanaotaka kujitenga.

Sababu za kuzuka mapigano ya wiki iliyopita haifahamiki, lakini wachambuzi wanasema sehemu kubwa ya wakazi wa kusini mwa Yemen hawana tena imani na Rais Mansour na hasa bado hawaridhiki na hali kwamba walilazimishwa kuungana na kaskazini kati kati ya miaka ya 1970.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu, Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG