Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Machi 04, 2024 Local time: 01:16

Viongozi wa IGAD wakutana Ethiopia


Viongozi wa IGAD wanatarajiwa kukutana tena Jumanne kuzungumzia mzozo wa Sudan Kusini
Viongozi wa IGAD wanatarajiwa kukutana tena Jumanne kuzungumzia mzozo wa Sudan Kusini
Viongozi wa jumuia ya maendeleo ya Afrika mashariki na pembe ya Afrika- IGAD, wanapanga kukutana mjini Addis Ababa, Ethiopia, Jumanne kujadili namna ya kuimarisha usalama na amani katika kanda yao pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa kati ya mataifa hayo sita. Hata hivyo maafisa walioko karibu na mkutano huo wanasema suala la ugomvi wa Sudan Kusini litakua juu katika ajenda yao.

Maafisa wa IGAD wanasema viongozi watakaoshiriki watajaribu kutafuta njia za kupata suluhisho kwa mzozo huo wa Sudan Kusini na kadhalika namna ya kukabiliana na vitisho vinvyotolewa na kundi la wanamgambo wa ki-Islamu la Al-Shabab kutoka Somalia.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani ilitangaza Jumatatu kwamba mjumbe maalum kwa Sudan na Sudan kusini, Donald E. Booth pamoja na mshauri mkuu wa masuala ya kisheria wa wizara hiyo Thomas A. Shannon, wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa viongozi wa IGAD. Mkutano huo wa viongozi utafanyika baada ya Rais Salva Kiir kukutana na kiongozi wa upinzani Riek Machar.

Hata hivyo waziri wa masuala ya nchi za nje wa Sudan Kusini, Barnaba Marial Benjamin, anasema mkutano kati ya Rais Kiir na Bwana Machar unafanyika kama sharti lililotolewa na wapatanishi kwamba viongozi hao waone kwa kiwango gani makubaliano ya kusitisha uhasama yametekelezwa hadi sasa.

Mkutano wao unafanyika mwezi mmoja baada ya wote bwana Kiir na bwana Machar kutia saini mkataba huko Ethiopia kuahidi tena juu ya utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha uhasama waliokubaliana awali na huku majadiliano yanaendelea baina ya pande hizo mbili.

Wote serikali na waasi hivi karibuni walilaumiana kwa kuhujumu makubaliano ya kusitisha uhasama. Lakini bwana Benjamin anasema waasi ndio wa kulaumiwa kwa tukio la kushambulia vituo vya serikali. Mzozo huo umepelekea maelfu ya watu kupoteza makazi yao.

Bwana Benjamin anasema serikali ya Juba inadhamira ya dhati kuendelea na mazungumzo ya amani, lakini anatoa wito kwa viongozi wa kikanda kushinikiza waasi kuyachukulia kwa dhati majadiliano hayo. Ghasia huko Sudan Kusini zilizuka baada ya Rais Salva Kiir, kutoka kabila la Dinka, kumshutumu Makam Rais wa zamani Riek Machar anayetoka kabila la Nuer kujaribu kumpinduwa. Machar anakana tuhuma hizo, lakini hatimae aliunda kundi la waasi kupigana dhidi ya utawala wa Juba.
XS
SM
MD
LG