Vikosi vya Umoja wa Afrika nchini Somalia vimesema kuwa wanajeshi wake wameuwa zaidi ya wanamgambo 100 wa kundi la Al-Shabab walioshambulia kituo cha kijeshi mapema leo.
Wakazi wanasema kuwa bomu la kwenye gari lililipuka kwanza nje ya lango la kituo cha kijeshi cha Ethiopia kijijini humo kilichoko takriban kilomita 260 kasakazini mwa Mogadishu na kisha baadae kufuatiwa na mashambulizi kutoka kwa wanamgambo waliokuwa wamejihami vikali.
Msemaji wa kikosi cha muungano cha AMISOM Kanali Joseph Kibet ameoambia VOA vikosi vya serikali kwa ushirikiano na vile vya Ethiopia vilizuia shambulizi hilo.
Radio rasmi ya Al-Shabab ya Andalus imesema kuwa wameuwa wanajeshi 43 wa Ethiopia wakati wa shambulizi hilo na pia kuharibu kituo cha kijeshi.
Tangu Juni mwaka uliopita, kundi la Al-Shabab limeshambulia vituo vitatu vya vikosi vya muungano AMISOM na kuuwa wanajeshi 54 wa Burundi mjini Leego, 19 wa Uganda eneo la Jannaale, na zaidi ya 100 kutoka Kenya kwenye eneo la El-Adde.