Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 30, 2024 Local time: 21:48

‘Vijana ni waamuzi wakuu katika uchaguzi mkuu Kenya’


Wanafunzi wakishiriki katika mafunzo kwenye kituo cha Teknolojia Nairobi, Kenya.
Wanafunzi wakishiriki katika mafunzo kwenye kituo cha Teknolojia Nairobi, Kenya.

Wakati Kenya inapoelekea kwenye uchaguzi mkuu, ikiwa zimebakia siku sita bila shaka kundi la vijana katika kupiga kura ni muhimu kuangaziwa.

Taifa la Kenya lina takriban watu milioni 42 kulingana na takwimu za sensa ya mwaka 2009. Katika idadi hiyo vijana walio na umri kati ya miaka 18 na 35 ni asilimia 60.

Takwimu kuhusu wapiga kura zilizotolewa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya, IEBC , zinaonyesha kuwa kati ya watu milioni 19 waliosajiliwa kupiga kura mwaka 2017 vijana ni milioni 9.9.

Kati ya maeneo ambayo yana idadi kubwa ya vijana miongoni mwa wapiga kurani Nairobi, Kiambu Nakuru Kakamega na Meru. Hii inadhihirisha umuhimu wa kundi hili katika uchaguzi mkuu wa taifa la Kenya.

Wadadisi wa maswala ya kisiasa wanasema kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kuamua nani ataongoza taifa hili.

Idadi ya vijana waliojitokeza kujisajili kupiga kura imeongezeka awamu hii ikilinganishwa na awamu zilizopita ambapo vijana walidai kutatizwa kutokana na ukosefu wa vitambulisho.

Kwa missing hiyo vijana wamevutia wanasisasa ambao wanawatizama kama kiungo muhimu kunyakua ushindi wa viti mbali mbali vya kisiasa.

Wakati huo huo idadi ya vijana ambao wanagombea nyadhifa za kisiasa kuanzia nafasi ya uwakilishi wa wadi mpaka nafasi ya useneta nayo imeongezeka ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.

Miongoni mwa wanaogombea viti vikuu vya kisiasa nchini ni kama Eliud Sifuna na Johnstone Sakaja wanaogombea kiti cha useneta katika kaunti ya Nairobi.

Halima Anwar ambaye anagombea kiti cha mwakilishi wa wanawake kaunti ya Mombasa na mpinzani wake Sadaf Deen ambaye aliachana na uwana mitindo na kuingia katika siasa.

Lakini aliyevutia wakenya wengi na umaarufu wake kuongezeka ni Eliud Muthiora Kariara mgombea mwenza wa Japheth Kavinga mgombea wa kujitegemea katika kiti cha urais.

Na kwa vile kila mwamba ngoma huvutia kwake kila mwanasiasa Kenya amebunisera za kuwavutia vijana.

Hili limedhihirika wazi kwenye manifesto za vyama vya Jubilee na Muungano wa NASA ambao wote wameahidi kutoa ajira kwa vijana, huku elimu ya juu ikiangazwa. Katika miaka ya nyuma wanasiasa wamewatumia vijana au kwa kununua kadi zao za kura na kuwanyima nafasi ya kufanya maamuzi wenyewe au kuwafadhili kuzua rabsha lakini mwishoe kubakia na majuto.

Mwaka huu mambo yanaonekana kuwa tofauti huku vijana wakijaribu kutafuta nafasi yao baada ya hamasisho la kutosha.

Munira Khamisi mkereketwa wa maswala ya vijana anaelezea kuwa kutokana na ukosefu wa fedha na pia sera zinazowajali vijana wanajipata hatarini kutumiwa. Muungano wa bara Uropa ambalo limetuma waangalizi wake wa uchaguzi nchini Kenya limeonya uwezekano wa ghasia baada ya uchaguzi na kundi ambalo litaangaziwa sasa ni vijana.

Sio siri tena kuna uwezekano wa kuzuka ghasia na endapo hili litatokea kuna hatari itasababisha taswira ya kila mtu kupoteza haki yake na ni muhimu kila mtu kumpa mwenzake nafasi na haki ya kupiga kura.

Maafisa wakuu serikalini akiwemo kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani ya Nchi Fred Matian’gi na Inspecta Jenerali wa Polisi Joseph Boinet wamesisitiza kuwa idara za usalama zimejitayarisha kukabiliana na tukio lolote.

Wito huu umesisitizwa na msemaji wa polisi Charlce Owino ambaye katika kituo kimoja cha redio Mombasa aliangazia mpago wa serikali kukabiliana na ghasia haswa katika maeneo yaliotajwa kuwa hatari.

Lakini licha ya hilo vijana Kenya wanasema wako tayari kushiriki kikamilifu ikilinganishwa na hapo awali ambapo hawakupewa nafasi.

Katiba ya Kenya mwaka 2010 imebainisha uteuzi wa wabunge maalum katika mabunge yote ya kaunti, Seneti na bunge la kitaifa lazima vijana wapewe nafasi.

Kwa sasa macho yote yameelekezwa tarehe ya uchaguzi japo la msingi ni kuwa vijana wanasalia kundi muhimu katika uchaguzi wa taifa la Kenya.

Na hata kama uwezo wao wa kifedha kugombea viti mbali mbali ni mdogo idadi yao ni muhimu katika kufikia maamuzi ya busara katika uchaguzi wa Kenya.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Liberty Adede, Kenya

XS
SM
MD
LG