Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Januari 31, 2023 Local time: 15:53

Upinzani wamuonya Kabila kuhusu uteuzi wa waziri mkuu DRC


Rais Joseph Kabila

Upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamemuonya Rais Joseph Kabila kutokwenda kinyume na mkataba wa kisiasa kwa kumteua waziri mkuu nje ya utaratibu wa mkataba huo.

Msimamo huo umetolewa baada ya rais kabila kutangaza kuwa atateuwa waziri mkuu mpya mnamo masaa 48 baada ya kutokuwepo makubaliano baina ya chama tawala na upinzani.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa katika taarifa iliosainiwa na kiongozi wa vuguvugu la upinzani la RASAMBLEMENT, Felix Tshisekedi, imeeleza kuwa hatua ya Rais Kabila kuwa atachagua waziri mkuu mpya bila maridhiano ya upinzani ni ukiukaji mkubwa wa mkataba wa kisiasa.

Kiongozi huyo wa upinzani ameongeza kuwa hatua hiyo itahatarisha hali ya kisiasa nchini Kongo.

Mwandishi wetu ameeleza kuwa hata hivyo upinzani umesema uko tayari kuendesha mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Kabila.

Christophe Lutundula Apala kutoka vuguvugu la RASAMBLEMENT amesema kwamba hatua ya rais kabila imeonyesha wazi kwamba hana nia nzuri ya kisiasa, katika kutafuta suluhisho la mzozo uliopo hivi sasa.

“Rais Kabila ameenda kinyume na mkataba kwa sababu zifuatazo. Kwanza amesema atateua waziri mkuu mnamo masaa 48. Nimekumbusha kwamba chama chake kiliwahakikishia maaskofu kwamba hakutakuwepo uchaguzi wa waziri mkuu hadi hapo mazungumzo ya kitaifa yatakapokamilika,” amesema Apala.

“Pili mkataba wenyewe unaeleza kwamba uteuzi wa waziri mkuu utafanyika kufuatia mashauriano kati ya kiongozi wa upinzani na Rais Kabila,” ameongeza kusema.

Lakini baadhi ya wapinzani wanasema kuwa mpasuko ndani ya upinzani ndio uliosababisha rais kabila kuchukua hatua mpya ya kuendesha mwenyewe mashauriano na baadhi ya vyama vingine vya upinzani.

Mmoja wapo wa vigogo wa chama cha UPDS, Mpinzani Justine Bitakwira, waziri wa masuala ya Bunge, kwenye serikali ya mseto amesema kwamba wenzao wa RASAMBLEMENT lazima wawajibike.

“…tunawaomba watu wa UPDS, na RASAMBLEMENT waelewe ya kwamba hii nchi haikuwa ya Etienne Tshisekedi, na kana kwamba amemwachia mototo wake, sio hivyo kabisa. Tshisekedi alikuwa mwananchi kama watu wengine,” amesema kiongozi huyo wa upinzani.

Huku ikibakia siku mmoja kabla ya kuteuliwa kwa waziri mkuu mpya, juhudi za kisiasa na za kidiplomasia zinaendelea ili kuweko na makubaliano ya dakika za mwisho.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Saleh Mwanamilongo, DRC

XS
SM
MD
LG