Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Mei 20, 2024 Local time: 18:34

Utawala wa kijeshi nchini Mali wasimamisha shughuli zote za vyama vya siasa


Kiongozi wa kijeshi wa Mali (katikati) Kanali Assimi Goita, akihudhuria maadhimisho ya uhuru wa Mali mjini Bamako, Juni 18, 2023. Picha ya AP
Kiongozi wa kijeshi wa Mali (katikati) Kanali Assimi Goita, akihudhuria maadhimisho ya uhuru wa Mali mjini Bamako, Juni 18, 2023. Picha ya AP

Utawala wa kijeshi nchini Mali Jumatano uliamuru kusimamishwa kwa shughuli zote za vyama vya siasa, ukisema hatua hiyo inahitajika ili kudumisha usalama wa umma.

“Hadi itakapotolewa taarifa nyingine, kwa sababu za usalama wa umma, shughuli za vyama vya siasa na shughuli za aina ya kisiasa za mashirika ya kiraia zimesimamishwa nchini kote,” chini ya amri iliyotolewa na kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita, msemaji wa serikali alisema.

Amri hiyo imetolewa baada ya zaidi ya vyama 80 vya siasa na makundi ya kiraia kutoa taarifa ya pamoja tarehe 1 Aprili, wakiomba uchaguzi wa rais ufanyike “haraka iwezekanavyo” na kumalizika kwa utawala wa kijeshi.

Taifa hilo la Afrika magharibi limeongozwa na wanajeshi tangu mapinduzi ya mfululizo mwaka 2020 na 2021, huku hali ya usalama pamoja na mzozo wa kisiasa na kibinadamu ikizidi kuwa mbaya.

Mwezi Juni 2022, utawala wa kijeshi ulisema uchaguzi wa rais ungefanyika mwezi Februari na utawala kukabidhiwa kwa raia tarehe 26 Machi. Lakini uchaguzi uliahirishwa na uongozi wa kijeshi haukutangaza tarehe nyingine.

Msemaji wa serikali Kanali Abdoulaye Maiga amefafanua kusimamishwa kwa shughuli za vyama kwamba ni kutokana na “majadiliano yaliyokwama” wakati wa jitihada za mjadala wa kitaifa mwaka huu.

Sauti za upinzani zimenyamanzishwa kwa kiasi kikubwa chini ya utawala wa kijeshi.

Forum

XS
SM
MD
LG