Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 21:57

Utangulizi : Uganda inajitayarisha kwa Uchaguzi wenye ushindani mkali


FILE - Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha National Resistance Movement Yoweri Museveni akiwasalimia wafuasi wake wakati akiwasili katika mkutano wa kampeni mjini Entebbe, Uganda, Feb. 10, 2016.
FILE - Mgombea urais kwa tiketi ya chama cha National Resistance Movement Yoweri Museveni akiwasalimia wafuasi wake wakati akiwasili katika mkutano wa kampeni mjini Entebbe, Uganda, Feb. 10, 2016.

Uganda inajitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa rais na bunge hapo Januari 14 2021. Kuna wagombea 11 wanaopigania kiti cha rais ambapo Rais wa sasa Yoweri Museveni anagombea mhula wake wa sita.

Hii ni kwa sababu hakuna kizuizi cha mihula wala umri wa juu zaidi kwa wagombea wa rais nchini humo, hata hivyo umri wa chini ni miaka 18.

Kiongozi huyo wa muda mrefu, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mwanamuziki Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, pamoja na aliyekuwa kamanda wa jeshi, Gen. Mugisha Muntu, aliyekuwa waziri wa usalama Lt Gen Henry Tumukunde, Nobert Mao, John Katumba, Patrick Amuriat Oboi, Joseph Kabuleta, Fred Mwesigye, na aliyekuwa mwandishi wa habari Nancy Kalembe ambaye ni mwanamke pekee katika kinyanganyiro hicho.

Mpinzani mkuu wa rais Yoweri Museveni katika uchaguzi mkuu mara nne Dr.

Kiongozi wa upinzani Kiiza Besigye
Kiongozi wa upinzani Kiiza Besigye


, alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho akisema kwamba haina maana yoyote kuendelea kugombea urais wakati hakuna kile ametaja mara nyingi kama “uchaguzi huru na haki.” Besigye amesisitiza kwamba Museveni atafanya udanganyifu katika hesabu ya kura ili kusalia mdarakani.

Upinzani mkali dhidi ya Museveni

Wachambuzi wengi wa siasa Uganda na kote Afrika Mshariki, wanasema kwamba kinyang’anyiro cha urais ni kati ya rais Museveni na Bobi Wine, wote wakiwalenga sana vijana katika kampeni zao.

Rais Yoweri Museveni
Rais Yoweri Museveni

Kulingana na tume ya uchaguzi, jumla ya wapiga kura 17,658,527 wameandikishwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Januari 14 2021. Kuna vituo 34,344 vya kupigia kura.

Mgombea urais Bobi Wine
Mgombea urais Bobi Wine

Kulingana na sheria za uchaguzi nchini Uganda, mshindi wa kura za urais anastahili kupata asilimia 50 ya kura zote zilizopigwa pamoja na kura moja zaidi. uchaguzi unarudiwa katika duru ya pili endapo mshindi hapatikani katika duru ya kwanza lakini hali kama hiyo haijawahi kutokea katika historia ya Uganda.

John Katumba ndiye mgombea mwenye umri mdogo zaidi. Ana miaka 24. Yoweri Museveni ndiye mgombea mwenye umri wa juu zaidi, akiwa na miaka 76. Tofauti kati yao ni miaka 52.

Tarehe Muhimu katika uchaguzi wa Uganda 2021

Jan 11, 2021- Uchaguzi wa madiwani wanaowakilisha watu wazee

Jan 11, 2021–Uchaguzi wa madiwani wanaowakilisha walemavu

Jan 11, 2021 – Uchaguzi wa waakilishi wa vijana bungeni

Jan 14, 2021 – Uchaguzi wa rais na wabunge

Jan 17, 2021 – Kongamano la kitaifa la waakilishi wa watu wazee kuchagua waakilishi wao bungeni

Jan 17, 2021 – Kongamano la kitaifa la kuchagua waakilishi wa walemavu bungeni

Jan 17, 2021 – Kongamano la waakilishi wa wafanyakazi kuchagua waakilishi wao bungeni

Jan 20, 2021 – uchaguzi wa Meya na wenyekiti wa wilayani

Jan 21, 2021 – kongamano la kitaifa la vijana kuchagua waakilishi wake wa kike

Jan 25, 2021 – uchaguzi wa viongozi katika ngazi ya manispaa

Jan 29, 2021 – uchaguzi wa waakilishi wa wanajeshi bungeni

Idadi kubwa ya wagombea huru

Bunge la Uganda lina nafasi za wabunge 426. Wabunge 289 watachaguliwa moja kwa moja kuakilisha maeneo bunge, 112 wakilishi wa wanwake kutoka kila wilaya, na waakilishi wa makundi maalum 25 wakiweo vijana, wazee, na watu walevamavu. Lina pia wabunge wanaowakilisha wanajeshi.

Zaidi ya nusu ya wagombea wa viti vya bunge ni wagombea huru wasiokuwa na vyama vya kisiasa. Idadi hiyo ni wagombea 1,338.

Chama kinachotawala cha National resistance Movement - NRM kina wagombea wengi wa nafasi katika bunge (487), Forum for democratic change – FDC (281) National unity platform -NUP chake Bobi Wine (242) Democratic party – DP (120), Alliance for national Transformation ANT (116), Uganda people’s congress – UPC (42), Justice Forum – JEEMA (19) na vyama vingine vidogo vidogo 7 vikiwa na jumla ya wagombea 14.

Chama kinachotawala cha National resistance movement NRM, tayari kina wabunge 12 ambao wametetea nafasi zao bila kupingwa.

Waangalizi wa uchaguzi

Umoja wa Ulaya umesema kwamba hautatuma waangalizi wake kufuatilia uchaguzi mkuu wa Uganda kwa sababu mapendekezo yake baada ya uchaguzi wa mwaka 2016, hayakutiliwa maanani na serikali ya Uganda.

Kwa kawaida, Umoja wa Ulaya hutuma idadi kubwa ya waangalizi katika uchaguzi mbali mbali barani Afrika na sehemu zingine za dunia.

Kulingana na ripoti ya Umoja wa Ulaya ya mwaka 2018, serikali ya Uganda haikutia maanani mapendekezo yake yote 30 ya mwaka 2016 namna ya kuandaa uchaguzi ulio huru na haki.

Ripoti hiyo inasema kwamba hakuna pendekezo lolote limetekelezwa wala serikali kuonyesha nia ya kutaka kutekeleza.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kubuniwa kwa tume huru ya uchaguzi, polisi na maafisa wa usalama kuacha kutumia nguvu dhidi ya wagombea wa upinzani na kuweka mazingira ya wazi wakati kura zinahesabiwa.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG