Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 22, 2024 Local time: 12:02

Mattis Asema Marekani Haitashirikiana Kijeshi na Russia


Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis
Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Jim Mattis

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Jim Mattis amesema haiwezekani kabisa kuwepo ushirikiano wa kijeshi kati ya Marekani na Russia, akieleza kuwa haitokuwa sawa kutokana na “hali vile ilivyo” hivi sasa baina ya mataifa haya.

“Hatuwezi hivi sasa kushirikiana kijeshi. Lakini viongozi wetu wa kisiasa wataendelea kuwasiliana na kutafuta muafaka,” Mattis amesema hayo katika mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya NATO, Brussels, Ubelgiji.


Kabla ya ushirikiano wa kijeshi kufanyika, Russia lazima “ithibitishe” iko tayari kuheshimu sheria za kimataifa, Mattis amesema.

Russia Inataka Ushirikiano
Maoni ya Mattis yamekuja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergei Shoigu kusema Moscow “iko tayari kurejesha ushirikiano na Pentagon.”

Rais Donald Trump alimsifia kiongozi wa Russia, Vladimir Putin wakati wa kampeni na kuendelea kufanya hivyo baada ya kuchukua madaraka na amesema anapenda kuanzisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.

Marekani ilisitisha ushirikiano wake wa kijeshi na Russia mwaka 2014 baada ya nchi hiyo kuvamia eneo la Crimea nchini Ukraine.

Udukuzi wa Mitandao Waongezeka

Katika siku ya pili ya mazungumzo ya mawaziri wa NATO Alhamisi mjini Brussels, Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg amesema watazungumzia jinsi ya kuzuia kuongezeka kwa udukuzi wa mitandao dhidi ya serikali mbalimbali.

Mattis amesema anaamini NATO ina uwezo wa kupambana na tishio hilo la udukuzi wa mitandao, na amesema marafiki zake wamepokea ujumbe wake vizuri siku iliyopita kuhusu kushirikiana katika gharama za ulinzi.

“Tulizungumza kuhusu kuongezeka kwa uadui unaoukabili umoja wetu, na umechanganyika na vitisho dhidi ya demokrasia yetu na naona ni ushirikiano imara peke yake unaweza kutuondolea hatari hizi zinazoongezeka,” amesema Waziri huyo.

Ombi la Trump na Mattis

Trump na Mattis kwa pamoja wamezihimiza nchi nyingine za NATO kugharamia kifedha taasisi hiyo.

Mnamo Julai, wakati Trump akiwa mgombea urais alileta taharuki Ulaya kote alipopendekeza kuwa Marekani haitoshiriki kulinda wanachama wa umoja wa NATO ambao hawatoi michango yao.

Marekani Kupunguza majukumu yake

Siku ya Jumatano, Mattis amewatahadharisha mawaziri wa NATO kuwa Washington itapunguza majukumu yake” kwa umoja huo iwapo wanachama hawatatoa kiwango cha asilimia mbili ya pato la taifa kutoka kwenye bajeti zao.

“Marekani itatekeleza wajibu wake, lakini kama mataifa yenu hayataki kuona Marekani ikipunguza majukumu yake katika umoja huo, kila nchi inatakiwa kuonyesha kwa vitendo inasaidia kwa ajili ya ulinzi wetu wa pamoja,” Mattis amewaeleza mawaziri Jumatano katika mkutano wa faragha.

Mattis hajafafanua ni vipi Washington itabadilisha majukumu yake kwa umoja wenye wanachama 28.

Nchi Zinavyo Changia

Kati ya wanachama wa NATO, watano ambao wanatekeleza ahadi zao ni Ugiriki, ambayo inalipa takriban asilimia 2.5, na Poland, Estonia na Uingereza inalipa juu kidogo ya kiwango kinachotarajiwa cha asilimia mbili.

Kwa upande wa wale wasiofikisha kiwango kilichowekwa, Ujerumani inalipa asilimia 1.19 na wengi ikiwemo Canada, Itali na Spain zinalipa chini ya kiwango. Ufaransa inalipa chini kidogo ya asilimia mbili.
Marekani inalipa zaidi ya asilimia 3.6 ya pato lake la taifa.

XS
SM
MD
LG