Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Juni 22, 2024 Local time: 18:41

Ushindi wa Rais Macron waibua maoni mseto kuhusu mustakbali wa Ufaransa


Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron

Baadhi hawana furaha na ushindi huo huku wengi wakielezea afueni baada ya Macron kumshinda mpinzani wake wa siasa kali za mrengo wa kulia, Marine Le Pen huku wachambuzi wengi wakisema kwamba Ufaransa inaendelea kugawanyika licha ya ushindi wa muhula wa pili, wa Macron.

Zaidi ya robo ya wapiga kura hawakushiriki zoezi hilo huku asilimia 41.5 wakimpigia kura mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia mwenye kupinga sera za uhamiaji na mfumo wa siasa nchini humo Le Pen, mpinzani mkuu wa Macron.

Wafuasi wa Le Pen, anayepinga sera za kigeni, na mfumo wa siasa za sasa, wana hasira baada ya kushindwa.

Wanasema kwamba wanahisi kubaguliwa. Jean Mouette, mwenye umri wa miaka 63, anasema kwamba mabadiliko makubwa yanahitajika katika mfumo wa uchaguzi wa Ufaransa.

Marine Le Pen
Marine Le Pen

Mouette anaeleza: “Kuna watu wengi sana wanaohisi kwamba hawaja wakilishwa katika serikali na hili linastahili kushughulikiwa. Sijui kama ina maana tunahitaji kuandaa kongamano linalohusisha raia ili watoe maoni yao na kuwasikiliza, au kuandaa kura ya maoni licha ya hatari zinazokuja na kura hiyo, na serikali kushirikiana na upinzani.

Kuna njia nyingi na kuna kazi nyingi ya kufanya.”
Watu wengi wana matumaini kwamba muhula wa pili wa rais Macron utakuwa wa kutekeleza haki za kiraia, kupambana na umaskini na kuongeza mishahara kwa wafanyakazi, pamoja na kutambua maoni ya wapiga kura waliompigia kura badala ya Le Pen.

Mwalimu wa Muziki Valerie Jacquet amesema kwamba hii ina maana kwamba Wafaransa wana wasiwasi kuhusu maisha yao, mapato yao, usalama wao.
Jacquet anaeleza haya: Mwanya kati ya chama cha Le pen na cha Macron unapungua, na chama cha Le pen cha National Rally kinaendelea kupata umaarufu. Hii ina maana kwamba wafaransa wana wasiwasi kuhusu maisha yao, uwezo wao kununua bidhaa muhimu na hili ni jambo la kawaida na haki yao. Lakini nadhani kwamba sera za Le Pen zinagawa watu.

Macron, ambaye ni mtetezi mkubwa wa ujasiriamali, amelegeza kanuni za kuwafuta na kuwaajiri wafanyakazi pamoja na kuweka mazingira magumu sana ya watu kulipwa pesa kwa sababu ya kutokuwa na kazi.

Wakosoaji wake wanasema ameharibu ulinzi uliokuwepo wa wafanyakazi.
Mkurugenzi wa shirika linaloongoza kwa kukusanya kura ya maoni nchini Ufaransa la IPSOS, Brice Teinturier, ameiambia radio ya Ufaransa France Inter kwamba ushindi wa Macron ulikuwa wa haki na wala haukumdhalilisha Marine Le Pen, akiongezea kwamba La Pen amejiongezea umaarufu tangu uchaguzi wa mwaka 2017 alipokabiliana na Macron na kwamba chama chake kinaonyesha upinzani mkali dhidi ya serikali, nchini humo.

Mdahalo kati ya Rais Emmanuel Macron na mpinzani wake Marine Le Pen (Eric Feferberg/Pool Photo via AP, file)
Mdahalo kati ya Rais Emmanuel Macron na mpinzani wake Marine Le Pen (Eric Feferberg/Pool Photo via AP, file)

Teinturie amesema haya:“Uchaguzi huu hatimaye ulizingatia sana uwezo wa wagombea hao. Emmanuel Macron aliwavutia watu wanaofikiria kwamba ana uwezo wa kukabiliana na migogoro katika dunia ambayo imejaa misukosuko na uchaguzi huo ulizingatia sana vitisho vilivyopo na wala siyo maslahi ya taifa.”

Macron ni rais wa kwanza kushinda muhula wa pili madarakani nchini Ufaransa tangu ushindi wa Jacques Chirac mwaka 2002.

Macron anatarajiwa kuendelea kutekeleza sera zake za ndani na za nje, lakini huenda akapata wakati mgumu sana kupata idadi kubwa ya wabunge katika uchaguzi wa bunge.
End

XS
SM
MD
LG