Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Aprili 19, 2024 Local time: 11:49

Usalama waimarishwa Washington kabla ya kuapishwa Biden


Wafanyakazi wakijenga jukwaa la sherehe za kuapishwa rais katika viwanja vya Bunge la Marekani Washington, DC, on Disemba 1, 2020. (Photo by MANDEL NGAN / AFP)
Wafanyakazi wakijenga jukwaa la sherehe za kuapishwa rais katika viwanja vya Bunge la Marekani Washington, DC, on Disemba 1, 2020. (Photo by MANDEL NGAN / AFP)

Hali ya usalama imeimarishwa kuliko ilivyo kawaida katika mji mkuu wa Washington kabla ya kuapishwa kwa rais mteule Joe Biden hapo Januari 20.

Maafisa wa usalama na wale wa jiji hili kuu, wanatekeleza hatua za usalama ambazo hazijawahi kutekelezwa ili kuepusha vurugu kama iliotokea wiki iliyopita pale maelfu ya wafuasi wa Rais Trump walipovamia majengo ya Bunge la Marekani.

Idara za usalama za Marekani zinazo simamia usalama wa maandalizi ya sherehe za kuapishwa kwa Rais mteule Joe Biden wana dhamira ya kuepusha kutokea tena tukio lililoshuhudiwa wiki iliyopita katika majengo ya bunge ambako watu watano walifariki na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Maelfu ya maafisa wa kikosi cha ulinzi wa taifa kutoka majimbo kadhaa wanaletwa hapa Washington kuanzia mwisho wa wiki hii. Meya wa jiji hili Muriel Bowser anasema kwamba sherehe za kuapishwa Biden zinazusha changamoto ambazo hazijawahi kutokea kuanzia janga la COVID-19 hadi vitisho vya wafuasi wa itikadi kali.

Bowser anasema : "Watu wanaokuja kuandamana kwa njia za amani ni tofauti kabisa na wale watu tuliowaona wakivamia majengo ya bunge wiki hii. Na nina dhani itabainika kwamba watu hao waliovamia bunge waliandaliwa na kupata mafunzo.

Kupambana na ugaidi wa ndani ya nchi kunazusha changamoto za kipekee za kisheria anasema Said Javed Ali mtaalamu wa masuala ya kupambana na ugaidi katika chuo kikuu cha Michgan.

Ali anasema : "Unakabiliana na Wamarekani waliozaliwa na kukulia hapa nchini wenye haki za kulindwa chini ya katiba. Na wanafahamu mahala mipaka hiyo inapoanza na kumalizika kuhusiana na hadi kiwango gani cha harakati zao wanaweza kufanya kabla ya kugeuka kuwa uhalifu."

Hapo Jumanne wachunguzi wa idara ya upelelezi wa jinai FBI wamesema wamepokea karibu video na picha laki moja kama taarifa na kufungua kesi 160 katika uchunguzi wake kutokana na uvamizi huo.

Steven D’Antuono Naibu mkurugenzi wa FBI Washington anasema : "Tuna zingatia zaidi juu ya mashtaka ya uchochezi. Tuna chunguza na kuchukulia jambo hili kama juhudi za kupambana na ugaidi wa kimataifa au operesheni ya kupambana na ujasusi."

Akizungungumza na waandshi habari mapema wiki hii Rais mteule Joe Biden alisema hana uoga wowote wa kula kiapo nje kama ilivyo mila wakati wa kuapishwa kwa rais Marekani.

Biden alisema : "Siogopi, na ninadhani ni muhimu sana kwamba kuna hatua za dhati zinachukuliwa kuwawajibisha hawa watu wanaohusika katika uchochezi, kutisia maisha ya watu, kuharibu mali ya umma na kusababisha uharibifu mkubwa.

Kwa wiki kadhaa maafisa wa usalama wamekuwa wakifuatilia harakati kwenye mitandao ya wanaharakati wenye itikadi kali za mrengo wa kulia na wazungu wabaguzi wa rangi wakihamasisha watu kuhusiana na shambulizi la Januari 6 dhidi ya majengo ya bunge. Hivi sasa maafisa hao wanazingatia katika kujitayarisha kukumbana na ghasia zaidi kuelekea siku ya sherehe za kuapishwa rais.

XS
SM
MD
LG