Shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa – UNHCR - linasema idadi ya watu ambao wamekimbia mkoa wa Abyei wenye mzozo nchini Sudan imefikia 100,000.
Msemaji wa Kamishna wa masuala ya wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Fatounata Lejeuna-Kaba, aliiambia Sauti ya Amerika-VOA, kwamba wengi wao wanatafuta hifadhi ya kisiasa katika jimbo la Warrap, kusini mwa Abyei.
Wakimbizi wengi walianza kukimbia eneo la mpaka wa kaskazini na kusini mwezi uliopita, baada ya majeshi ya kaskazini kudhibiti kimabavu mkoa wa Abyei.
Sudan Kusini inajiandaa kujitangazia uhuru wake kutoka kaskazini, Julai 9, na pande hizo mbili hazijakubaliana juu ya hali ya baadaye ya eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.
Khartoum inakataa wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalowataka kuyaondoa majeshi yake.
Maafisa wana khofu mivutano inayojirudia inaweza kuiingiza Sudan katika vita mpya ya wenyewe kwa wenyewe.
Sudan kaskazini na kusini walipigana kwa miaka 21 kabla ya mgogoro kumalizika kufuatia mkataba wa amani wa mwaka 2005.
Jumatatu, ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan iliyataka majeshi yenye silaha ya kaskazini kusitisha mashambulizi huko Abyei, kuwaachia raia waliowashikilia katika vizuizi vyao na kuruhusu njia zisizo na masharti na salama kwa watu wenye kuhitaji msaada wa kibinadamu.
UNHCR yasema watu 100,000 wakimbia Abyei
