UNDP yazindua ripoti ya chakula Afrika
Shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP ijumaa limezindua ripoti ya maendeleo kwa afrika na kutaja tatizo la njaa ni msamiati uliokosa ufumbuzi wa muda mrefu na hivyo imehimiza mapinduzi ya fikra ili kukwamua janga hilo.
Ripoti hiyo ambayo imebeba dhima isemayo kuelekea kwenye mustakabali wenye uhakika wa chakula, imeeleza kuwa ongezeko endelevu kwenye uzalishaji chakula na lishe bora ndiyo vichocheo vya ukuaji katika kujitosheleza kwa chakula na maendeleo ya binadamu.
Ripoti hiyo ambayo ni ya kwanza kutolewa barani afrika, imeelezea hali halisi ya ukosefu wa chakula katika bara hili na eneo liliko kusini mwa Jangwa la sahara. Kwa mujibu wa takwimu rasmi zilizopatikana kwenye ripoti hiyo, kutokana na kukithiri kwa tatizo hilo la njaa, kuna zaidi ya mtu mmoja katika kila waafrika wanne kukabiliwa na tatizo la upungufu wa lishe .
Ripoti hiyo imezishambulia sera zinazotekelezwa na dola za afrika, ikisema kuwa haziko sahihi na wala hazitekelezeki. Kadhalika imetaja udhaifu unaopatikana kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo zile zinazosimamia maamuzi.
Akitambua umuhimu wa ripoti hiyo, Naibu waziri wa fedha Bi Janet Mbene alisema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa shirika la umoja wa mataifa linalohusika na maendeleo kuchapisha ripoti inayoangazia bara la afrika pekee. Wataalamu walioandaa ripoti hiyo wanasema kuwa pamoja na rasilimali nyingi zinazopatikana ndani ya bara hili, lakini hata hivyo limeendelea kusalia nyuma.
Inasisitiza haja ya kufanyika mapinduzi ya kifikra ili kuliwezesha bara hili kusonga mbele na kuondokana na baa la njaa.
Hata hivyo baadhi ya wataalamu wa mambo wanaweka matumaini yao katika siku za usoni, akiwemo mtaalamu huyu kutoka UNDP.
Ili kufikia usalama wa chakula, ripoti inazitaka nchi za afrika kutetea kwa pamoja mipango ya kimaendeleo huku ikizimulika kwa makini sera zake.