Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Februari 25, 2024 Local time: 11:49

UN yapitisha jina jipya mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi


Ramani ya Rwanda
Ramani ya Rwanda

Umoja wa Mataifa (UN) umepitisha kwa kauli moja uamuzi wa kubadili jina la mauaji ya Rwanda kwa kupewa jina la mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya watutsi.

Awali mauaji hayo yalikuwa yakiitwa mauaji ya kimbari ya Rwanda kama ambavyo imekuwa ikifahamika.

Rwanda imepokea kauli hiyo kwa pongezi kutokana na mauaji hayo kuonekana mara nyingi yakipotoshwa kwa kuyataja kinyume na yalivyokuwa.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa hadi sasa imepita miaka 24 baada ya kufanyika mauaji ya kimbari yaliyolenga jamii ya watutsi nchini Rwanda.

Lakini tangu mwaka 1994 yamekuwa yakitajwa na jamii ya kimataifa kama mauaji ya kimbari ya Rwanda.

Manusura na serikali kwa ujumla wamekuwa wakisema kwamba kuyapa jina hilo mauaji hayo kunapotosha ukweli au uhalisia wake kwa sababu jina halionyeshi hasa mauaji hayo yaliwalenga kina nani.

Hata hivyo kwa kipindi chote hicho jamii ilionekana kulipokea hilo kwa shingo upande.

Lakini sasa kwa kauli moja Baraza la Usalama la UN limepitisha mabadiliko hayo na kuyataja mauaji hayo kama mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi nchini Rwanda.

Serikali ya Rwanda imesema kuwa imepokea kauli hiyo kwa mikono miwili.

Dr Jean Damascene Bizimana ni mwenyekiti wa tume ya taifa ya kupambana na mauaji ya kimbari na anaeleza:

“Tumepokea kauli hiyo kwa furaha kubwa,imepita miaka 24 tukiomba umoja wa mataifa kuachana na matumizi ya jina potofu ambalo halikuwa na uhalisia wa kile kilichofayika hapa,ni vema sasa kama hatimaye wameweza kutambua kuwa jina lililokuwa likitumiwa lilikuwa batili."

Hata hivyo amesema kwamba awali baraza la usalama la UN liliomba mataifa ya ulimwengu kuridhia ombi hilo la Rwanda lakini mataifa yakaendelea kukaidi mwito huo.

Kwa mujibu wa Dr Bizimana, mnamo mwaka 2014 baraza la usalama lenyewe liliyataka mataifa yote ya ulimwengu kuanza kutumia jina hilo baada ya kupitisha azimio nambari 2150 ambalo liliainisha ni sehemu gani ya wanaanchi wa Rwanda waliofanyiwa mauaji ya kimbari maana jina la awali lilikuwa halionyeshi hasa mauaji hayo yaliwalenga akina nani.

Ni vyema sasa kuwa UN ambayo inajumuisha mataifa yote ya ulimwenguni kulitambua hilo na kukosoa kosa hilo.

Hata hivyo kwa upande mwingine,hatua hii imefikiwa huku kukiendelea na sehemu nyingine ya kutokubaliana juu ya idadi ya watu waliouawa wakati huo.

UN unataja idadi ya watu laki nane huku serikali ya Rwanda ikishikilia watu waliouawa wakati huo walikuwa zaidi ya milioni moja.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Sylvanus Karemera, Rwanda.

XS
SM
MD
LG