Mlinda Amani kutoka Chad aliwapiga risasi na kuuwa wenzake wawili na kumjeruhi mwingine, katika shambulizi kaskazini mwa Mali.
Mwanajeshi mmoja alikamatwa kufwatia shambulizi hilo la Jumamosi huko Tassalit katika mkoa wa Kidal. Msemaji wa Umoja Mataifa Radhia Achouri alisema hakukuwepo na azma kwa shambulizi hilo na uchunguzi ungali unafanyika.
Hilo lilikuwa shambulizi la pili katika kipindi cha chini ya wiki tatu. Hapo Februari 25 mjini Kidal, mwanajeshi miongoni mwa vikosi vya Chad, alimuuwa kamanda na daktari mmoja wa Umoja Mataifa, baada ya wiki kadhaa za mivutano dhidi ya hali za maisha na malipo.
Katika miaka ya karibuni, dazeni kati ya wanajeshi elfu 2 wa Chad, wameondoka kutokana na hali ya maisha na kutokulipwa mishahara.
Tume ya Umoja Mataifa nchini Mali ilipelekwa mwezi July mwaka 2013, katika juhudi za kuwaondoa wanamgambo wa kiislamu ambao walikuwa wameteka sehemu kubwa za kaskazini mwa Mali. Tume hiyo imekuwa mojawapo wa tume hatari zaidi kwa wawalinda amani wa Umoja Mataifa, na imeshambuliwa mara kwa mara na wanamgambo nchini Mali.
Februari wanamgambo walishambulia kambi ya walinda amani wa Umoja Mataifa mjini Kidal, na kuuwa takriban wanajeshi 6 na kujeruhi wengine takriban 30.