Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 25, 2024 Local time: 15:18

UN: Idadi ya maambukizo ya HIV yapungua Afrika


Kampuni ya kisayansi ya Gilead, California nchini Marekani inayotengeneza kidonge cha Truvada ambacho ni moja ya dawa zinazotumika kwa watu wanaoishi na HIV
Kampuni ya kisayansi ya Gilead, California nchini Marekani inayotengeneza kidonge cha Truvada ambacho ni moja ya dawa zinazotumika kwa watu wanaoishi na HIV

Ripoti ya UN yasema maambukizo ya HIV barani Afrika yamepungua kwa asilimia 26, lakini ugonjwa huo bado ni tishio barani humo

Umoja wa Mataifa unasema idadi ya maambukizo mapya ya HIV katika nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara imepungua kwa zaidi ya asilimia 26 tangu mwaka 2006, lakini maeneo hayo yangali ni yale yaliyoathirika vibaya sana kuliko sehemu nyingine yeyote ya dunia kutokana na janga hilo.

Katika repoti iliyotolewa Jumatatu, Idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia ukimwi- UNAIDS, inaeleza kwamba japokuwa idadi ya maambukizo imeshuka, nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara bado zinakabiliwa na asilimia 70 ya maambukizo mapya duniani kwa mwaka jana.

Eneo hilo ni makazi ya theluthi mbili ya walioambukizwa na HIV kote duniani, licha ya kuwa ni asilimia 12 ya idadi ya wakazi wote duniani. Ripoti inasema Afrika kusini ina idadi kubwa ya watu wanaoishi na ukimwi duniani, ikikadiriwa wanafikia milioni 5.6.

Umoja wa Mataifa unasema idadi ya watu wanaokufa kutokana na ukimwi barani Afrika imekuwa ikishuka tangu mwaka 1998 kwa sababu ya huduma bora za kupata dawa bure zinazorefusha maisha.

Ripoti inaelezea kushuka kwa maambukizo mapya ya HIV kunatokana na mabadiliko ya tabia za ngono, kuongezeka kwa matumizi ya mipira ya kujamiiana-kondom, na watu wanasubiri muda mrefu kabla ya kuanza tendo la kujamiiana.

Umoja wa Mataifa unasema kwamba maambukizo mapya ya HIV duniani kote yameshuka kwa asilimia 21 tangu mwaka 1998, huku idadi ya vifo vinavyotokana na ukimwi imeshuka kwa kiasi kama hicho tangu kufikia kilele mwaka 2005.

Ripoti inasema kumekuwepo na muongezeko mkubwa wa watu wanaopatiwa huduma za dawa za kurefusha maisha katika nchi zenye pato la chini na la kati tangu mwaka 2009, na kwamba tiba inajukumu kubwa katika kupunguza kasi za maambukizo mapya.

XS
SM
MD
LG