Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Machi 25, 2023 Local time: 16:08

Mizinga yapigwa karibu na kituo cha UN Sudan


Milipuko mikubwa ya mizinga imepigwa karibu na kituo cha Umoja wa Mataifa nchini Sudan

Maafisa wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan wanasema mizinga ililipuka karibu na kituo chao huko Agos wakati mivutano ikiendelea kati ya kaskazini na kusini juu ya hali ya baadae ya mkoa wa Abyei unaogombaniwa.

Msemaji Kouider Zerrouk aliiambia Sauti ya Amerika kwamba mizinga sita ilipigwa ndani ya kilomita 150 za eneo la Umoja wa Mataifa hapo Ijumaa.
Zerrouk alisema kuna taarifa zinazotofautiana kuhusu mahali mizinga hiyo ilikotokea kama upande wa majeshi ya Sudan kaskazini au kundi la People’s Liberation Army la Sudan kusini.

Msemaji huyo alizitaka pande zote kusitisha hatua za kijeshi katika mkoa wa Abyei na alisema hali ya kibinadamu katika eneo hilo ilikuwa mbaya.
Sudan kaskazini ililikamata kimabavu eneo lenye utajiri wa mafuta la Abyei mwezi uliopita, na kufanya mpango wa Sudan kusini uwe mgumu kujitangazia uhuru rasmi hapo Julai 9.

Pande hizo mbili bado hazijakubaliana juu ya upande upi utalipata eneo lenye rutuba lililopo katika mpaka wa kaskazini na kusini.

Viongozi wa Sudan kaskazini na kusini, Ijumaa walianza mazungumzo ya kutatua masuala yanayowakabili kabla ya nchi hiyo kugawanyika kuwa mataifa mawili.

Washiriki wa mkutano huko Addis Ababa nchini Ethiopia wameambiwa na wapatanishi kuwa ni lazima waendelee kufanya kazi hadi makubaliano kati ya kaskazini na kusini yamefikiwa.

Wakati huo huo shirika la mpango wa chakula Duniani-WFP lilisema Ijumaa kwamba mapigano ya kaskazini na kusini katika jimbo la Kordofan kusini yamekwamisha juhudi za kuwafikia maelfu ya watu ambao wanahitaji msaada wa chakula.

XS
SM
MD
LG