Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 10, 2023 Local time: 16:18

Wachunguzi wa UN wagundua zaidi ya miili 50 katika kaburi moja


Eneo lililogunduliwa kuzikwa zaidi ya miili 50 ya watu katika kaburi moja huko Yopougon mjini Abidjan, Mei 4,2011
Eneo lililogunduliwa kuzikwa zaidi ya miili 50 ya watu katika kaburi moja huko Yopougon mjini Abidjan, Mei 4,2011

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanasema wamegundua kaburi la jumla nchini Ivory Coast lililozikwa zaidi ya miili 50 ya watu.

Maafisa wa ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wamesema leo Jumatatu kwamba kaburi hilo liligunduliwa katika wilaya ya Yopougon mjini Abidjan, mji mkuu wa kibiashara nchini humo.

Wakazi wa eneo wanasema waathirika waliuwawa April 12 wakati watu wenye silaha waliokuwa watiifu kwa Rais wa zamani Laurent Gbagbo walipowavamia wafuasi wa Rais mpya wa nchi hiyo, Alassane Ouattara.

Majeshi yanayomuunga mkono Ouattara yalimkamata bwana Gbagbo siku moja kabla, na kumaliza matatizo ya kisiasa yaliyochochewa wakati bwana Gbagbo alipokataa kushindwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika Novemba mwaka jana.

Ofisi ya haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa ilitangaza wiki iliyopita kwamba inachunguza ripoti kuhusu kaburi la jumla huko Yopougon na uwezekano wa mauaji ya raia yaliyofanywa na pande zote mbili.

Mamia ya watu waliuwawa wakati wa miezi minne ya ghasia za kisiasa nchini Ivory Coast. Umoja wa Mataifa inasema kiasi cha watu milioni moja wamekoseshwa makazi.

Rais Ouattara ameapa kuunda tume ya ukweli na maridhiano na kuwawajibisha wote waliohusika na vitendo vya kihalifu wakati wa mzozo wa kisiasa.

Ofisi ya bwana Ouattara inasema Rais ataapishwa rasmi katika mji mkuu wa kisiasa wa Yamoussoukro, Mei 21.

XS
SM
MD
LG