Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Septemba 29, 2023 Local time: 14:23

Umoja wa Mataifa washtumu mauaji Sudan Kusini


Wananchi wa Sudan Kusini wakitoroka machafuko nchini mwao. Desemba, 2013

Umoja wa Mataifa unashtumu matumizi ya matangazo ya kituo kimoja cha radio kinachomilikiwa na waasi kwa kuchochea mauaji na ubakaji.

Tume ya Umoja wa Mataifa iliyoko Sudan Kusini inasema waasi waliuwa mamia ya raia katika mashambulizi yaliyochochewa na ukabila, walipoteka mji wa Bentiu wiki jana.
Tume hiyo imeshtumu vikali mauaji hayo dhidi ya raia, ambayo yalifanywa kwa misingi ya kitaifa na kikabila.

Katika taarifa tume hiyo inayojulikana kwa kifupi kama UNMISS, ilisema zaidi ya wananchi 200 waliripotiwa kuuawa na zaidi ya 400 kujeruhiwa katika msikiti wa Bentiu ambapo walikuwa wamekimbilia kutafuta hifadhi.

Aidha ripoti hiyo ilielezea wapiganaji wa kundi la waasi ambao pia wanajulikana kama SPLA-Upinzani, waliwatenga watu kwa misingi ya utaifa wao au makabila yao na kuwasindikiza wengine katika maeneo salama na kisha kuwaua wengine.
Mashambulizi sawa na hayo yaliripotiwa katika Kanisa la Katoliki na kwenye uwanja unaotumiwa na shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na pia katika hospitali ya Bentiu. Wasudan wa kabila la fur kutoka mkoa wa Darfur pia walilengwa katika mauaji hayo.

Umoja wa Mataifa pia ulishtumu matumizi ya matangazo ya kituo kimoja cha radio kinachomilikiwa na waasi kwa kuchochea mauaji na ubakaji.Msemaji wa tume hiyo ya walinda amani Nick Birnback aliiambia Sauti ya Amerika kuwa tume ya UNMISS imeongeza walinda amani katika mji wa Bentiu na maeneo mengine yaliyoshambuliwa na waasi .

Mgogoro wa Sudan Kusini ulizuka Desemba baada ya wanajeshi watiifu kwa rais Salva Kiir na waasi walioegemea upande wa makamu rais wa zamani Riek Machar kuanza kupigana.Ghasia hizo sasa zimesababisha zaidi ya wananchi milioni moja kutoroka manyumbani mwao.
XS
SM
MD
LG