Afisa wa ngazi ya juu anayehusika na uhalifu wa kingono huko Umoja wa Mataifa anasema waasi waliohusika katika ubakaji wa wanawake wapatao 500 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hivi karibuni wanajulikana na watafikishwa mahakamani.
Katika mahojiano na Sauti ya Amerika Alhamisi Margot Wallstrom alisema Umoja wa Mataifa unajua majina na hata sura za viongozi wa ubakaji huo uliochukua siku nne katika vijiji 13 katika jimbo la Kivu Kaskazini. Alisema "wakati huu" watafikishwa mbele ya sheria.
Wallstrom alisema waliofanya vitendo hivyo walitoka katika kundi la FDLR, kundi la waasi Wahutu waliotokea Rwanda, na kundi moja la Mai Mai la mashariki mwa Congo.
Alisema kuwa ubakaji unatumika "kama silaha katika vita" huko mashariki mwa DRC na kwamba baraza la usalama linatafakari hatua dhidi ya makundi hayo.
Ubakaji ni tatizo sugu mashariki mwa Congo, ambako serikali imeshindwa kudhibiti waasi na makundi ya wanamgambo.
Umoja wa Mataifa unasema karibu vitendo elfu 15 vya ubakaji vinaripotiwa Congo kila mwaka.