Bosman alifariki Jumanne baada ya kuugua kwa muda mfupi, akiwa na umri wa miaka 50. Kwa mujibu wa taarifa ya shirika la habari la AP, familia ya Bosman imesema kwamba alifariki baada ya kuugua kwa muda mfupi akiwa nyumbani kwake akizungukwa na wanafamilia.
Bosman ambaye alizaliwa kwenye kitongoji cha Soweto amesifiwa na wengi kama mwanamuziki aliyeweza kucheza mitindo ya aina mbali mbali. Chama tawala cha ANC kimetoa rambi rambi zake kikisema kwamba muziki wa Afrika Kusini utapungukiwa bila uwepo wake.
Mwanamuziki mkongwe wa jazz kutoka nchini humo Sipho 'Hotstix' Mabuse pia alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kutoa pole, baada ya kifo hicho cha Bosman.Album yake ya kwanza ya Tranquility ilitolewa mwaka 1999 na ikashinda tuzo ya mwanamuziki bora chipukizi mwaka huo Afrika Kusini. Baadaye alishinda nyingine kwenye tuzo za muziki za Afrika Kusini pamoja na kuteuliwa mara 11.
Aliwahi pia kushinda tuzo mbili za kote Afrika za Kora, wakati pia akitumbuiza watu kote ulimwenguni. Katika maisha yake ya kimuziki,Bosman aliwahi kushirikiana na wanamuziki mashuhuri kama vile marehemu Hugh Masekela, Sibongile Khumalo, Moses Molelekwa na pia marehemu Oliver Mutukudzi kutoka Zimbabwe.
Mwaka uliopita alichaguliwa kwenye bodi ya muziki ya Afrika Kusini, inayolinda haki za wasanii. Taarifa zaidi kuhusu mipango ya mazishi yake bado hazijatolewa. Sisi pia tunatoa pole zetu kutokana na kifo cha mwanamuziki Gloria Bosman.
Facebook Forum