Baraza la mawaziri nchini Uganda limeondoa pendekezo la sheria mpya, iliyolenga kubadilisha sheria ya sasa inayowapa wapiga kura fursa ya kumchagua meya wa jiji la Kampala.
Hii ni baada ya maandamano ya raia jijini Kampala kupinga sheria hiyo mpya, ilioasilishwa bungeni na Waziri mdogo katika ofisi ya Rais, Frank Tumwebaza, ikitaka meya wa jiji la Kampala kuteuliwa na madiwani na wala sio kupigiwa kura na raia.
Wananchi wa Kampala walilazimika kuandamana hivi majuzi kupinga sheria hiyo katika tukio ambalo lilisababisha mwandishi mmoja wa habari kujeruhiwa kwa risasi.
Chama tawala cha NRM kimekuwa kikishutumiwa kwa kujaribu kufanya mbinu kwa miaka mingi ili kuweza kudhibiti uchaguzi wa meya wa jiji hilo, kitu ambacho kitakihakikishia chama hicho udhibiti wa jiji hilo muhimu katika uchumi na siasa za Uganda.