Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Julai 18, 2024 Local time: 15:03

Kura ya Brexit yaendelea kuzua mzozo Uingereza


Waziri wa Umoja wa Ulaya
Waziri wa Umoja wa Ulaya

Mzozo unaoikumba Uingereza ulionekana kuongezeka Jumatatu huku maafisa wa Umoja wa Ulaya wakitafuta mbinu za kukabiliana na wasiwasi uliokithiri baada ya wapiga kura wa nchi hiyo kuamua kwamba wataondoka Umoja wa Ulaya, hatua ambayo imeitumbukiza Uingereza katika hali ambayo imetajwa na wengine kama iliyo mbaya zaidi tangu vita vya pili vya dunia.

Katika jitihada za kusitisha kuyumbayumba katika masoko ya fedha hii leo, Waziri wa Fedha wa Uingereza, George Osborne, alitoa taarifa mapema leo, iliyosema kuwa uchumi wa Uingereza una nguvu na kwamba nchi hiyo iko ytayari kufanya biashara na mataifa mengine.

George Osborne
George Osborne

Masoko ya bara Ulaya yalionekana kuathirika leo asubuhi, hata ingawa hayakupata pigo kama ilivyokuwa siku ya Ijumaa wakati ambapo soko la fedha la London liliteremka hadi asilimia nane kabla ya kuimarika kidogo na kusimamia kwa juu kidogo ya asili mia tatu. Pauni ya Uingereza pia ilianguka tena wakati wa soko ya mapema leo.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, anazuru miji ya Brussels na London hii leo, safari ambayo itakuwa ya kwanza kwa afisa wa ngazi za juu wa serikali ya Marekani katika miji hiyo miwili, tangu Uingereza kupiga kura ya kujitenga na Umoja wa Ulaya wiki jana, hatua ambayo imeleta wasiwasi mwingi kwa Washington.

Maafisa wa Marekani wanasema kuwa Kerry, ambaye ameongeza miji hiyo miwili kwenye ratiba yake ya safari, ambayo awali ilikuwa impeleke mjini Rome, ataelezea uungaji mkono wa Marekani kwa Uingereza, na kusisitiza umuhimu wa mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Ulaya, kusalia kwenye muungano huo.

Kerry alisema jana Jumapili kwamba Marekani inasikitishwa na kura hiyo ya Uingereza kuondoka kwenye Umoja wa Ulaya, lakini akaapa kwendelea na uhusiano wa karibu na na umoja huo ambao hivi karibuni utakuwa na mataifa 27 wanachama.

XS
SM
MD
LG