Hunt alisema dhamana ya mkopo wa Uingereza imekuwa muhimu kufanikisha msaada mkubwa wa dola bilioni 15.6 kwa Ukraine kwa kipindi cha miaka minne kutoka shirika la kimataifa la fedha (IMF). Waziri Hunt anashiriki mkutano wa IMF wa baada ya msimu wa baridi mjini Washington.
“Ufadhili huu utaongeza ustahimilivu wa uchumi wa Ukraine na kuimarisha kusimama kwake kidete dhidi ya Russia,” alisema katika taarifa.
Uingereza kufikia sasa imeahidi msaada wa jumla wa dola bilioni 8.1 kwa Ukraine tangu uvamizi wa Russia mwezi Februari mwaka 2022, na dhamana za hivi karibuni za mkopo zitasaidia kufadhili huduma za umma za Ukraine kama vile shule na hospitali, wizara ya fedha imesema.
Hunt amesema pia amekamilisha nyongeza ya dola milioni 670 kwa mfuko wa kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa IMF, na dola bilioni 3.3 kwa mfuko wa ustahimilivu na endelevu wa IMF, ambao unasaidia miradi ya nishati na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.