Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 23:18

Uhuru, Raila wanatarajia ushindi mkubwa


Wafuasi wa chama cha Jubilee (kushoto) na wale wa muungano wa NASA wanahuduria mikutano ya mwisho ya kampeni zao katika uwanja wa Afraha, Nakuru, na Uhuru Park, Nairobi siku ya Jumamosi.
Wafuasi wa chama cha Jubilee (kushoto) na wale wa muungano wa NASA wanahuduria mikutano ya mwisho ya kampeni zao katika uwanja wa Afraha, Nakuru, na Uhuru Park, Nairobi siku ya Jumamosi.

Wagombea wa urais nchini Kenya walikuwa na shughuli mbali mbali Jumapili zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumanne.

Rais Uhuru Kenyatta alijiunga na waumini kwenye makanisa mawili mjini Nairobi na kuwaomba Wakenya wa tabaka mbali mbali kudumisha amani wakati wa uchaguzi huo.

Kulingana na kanuni za tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC, ni kinyume cha sheria kufanya shughuli zozote za kampeni saa 48 kabla ya zoezi la uchaguzi kuanza.

Msemaji wa kampeni ya Kenyatta, baadaye mwanasiasa huyo alifanya mikutano kadhaa na viongozi wa chama chake na kuthibisha mawakala watakaowakilisha chama hicho katika vituo mbali mbali vya kupigia kura nchini kote.

Mapema Jumapili, Kenyatta aliwatakia Wakenya zoezi la upigaji kura lenye amani. "Uwe wa Imani ya kikriso, Kiislamu au yoyote nyingine, naomba tufanye uchaguzi kwa amani," alisema.

Raila na Uhuru wakati wa mikutano yao ya kampeni za mwisho.
Raila na Uhuru wakati wa mikutano yao ya kampeni za mwisho.

Naye mgombea kwa tikiti ya NASA, Raila Odinga, alikutana na baadhi ya wafuasi wake katika eneo la Karen na baadaye kufanya mikutano na viongozi wa mrengo wake na kutoa orodha ya maafisa wa kushughulikia kipindi cha mpito iwapo atashinda kwenye kinyang’anyiro hicho.

Viongozi hao wawili walifanya mikutano miwili ya mwisho siku ya Jumamosi ambayo ilihudhuriwa na maelfu ya watu. Odinga alikuwa kwenye bustani za Uhuru Park, mjini Nairobi, huku Kenyatta akiongoza mkutano wake katika uwanja wa Afraha Stadium, Nakuru, takriban kilomita 160 kutoka Nairobi.

Rais Uhuru Kenyatta ambaye anagombea urais kwa muhula wa pili alifanya mkutano wa mwisho wa kampeni siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Afraha Stadium, kaunti ya Nakuru. Aliongoza maombi na kuwataka Wakenya kupiga kura kwa amani.
Rais Uhuru Kenyatta ambaye anagombea urais kwa muhula wa pili alifanya mkutano wa mwisho wa kampeni siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Afraha Stadium, kaunti ya Nakuru. Aliongoza maombi na kuwataka Wakenya kupiga kura kwa amani.

Kenyatta aliongoza maombi ya amani na kuwataka Wakenya kujitokeza kwa wingi, huku Odinga pia akiwataka wafuasi wa NASA kupiga kura kwa amani.

“Naomba mtupe nafasi nyingine ili kuendelea na miradi tuliyoanzisha wakati wa muhula wetu wa kwanza,” alisema Kenyatta.

“Nawasihi pia muwachague wawaniaji wa nyadhifa zingine kwa tikiti ya Jubilee ili tuendeleze ajenda yetu katika bunge, kaunti na kwingineko,” aliongeza.

Mgombea mwenza wa Kenyatta, William Samoei Arap Ruto alisema waliamua kufanya mkutano wa mwisho mjini Nakuru kwa sababu “ndiko chama chetu cha Jubilee kilizaliwa.”

Naye Raila odinga, ambaye anawania urais kwa mara ya nne, aliambia halaiki ya wafuasi wake kwamba ako tayari kuchukua usukani. “Nimeona dalili kubwa za ushindi kwenye uchaguzi wa Jumanne,” alisema.

“Nawaalika nyote kwa karamu ya ushindi kwenye Ikulu siku ya Jumamosi,” aliongeza huku waliohudhuria wakishangilia.

Mgombea urais wa muungano wa National Super Alliance, Raila Odinga, ahutubia wafuasi wake katika bustani za Uhuru Park mjini Nairobi mnamo siku ya Jumamosi. Alisema yuko tayari kuhika usukani wa Kenya na kwamba ameona dalili kubwa za ushindi.
Mgombea urais wa muungano wa National Super Alliance, Raila Odinga, ahutubia wafuasi wake katika bustani za Uhuru Park mjini Nairobi mnamo siku ya Jumamosi. Alisema yuko tayari kuhika usukani wa Kenya na kwamba ameona dalili kubwa za ushindi.

Raila alisema iwapo NASA itaunda serikali, ufisadi utatokomezwa. “Nitaenda nchini Tanzania na kutafuta suluhisho la kimagufuli,” alisema, huku akiashiria kutumia mfano wa uongozi wa rais wa Tanzania, John Pombe Maufuli – ambaye ni rafiki yake wa siku nyingi – kama kigezo cha kupambana na ulaji rushwa.

Mgombea mwenza, Stephen Kalonzo Musyoka, alisema polisi hawasemai ukweli kuhus kifo cha aliyekuwa naibu mkurugenzi wa idara ya mawasiliano na teknolojia kwenye tume ya IEBC, Chis Msando, ambaye mwili wake ulipatikana katika chumba cha kuhifadhi miti cha City, wiki moja iliyopita, baada ya afisa huyo kuripotiwa kupotea siku mbili kabla ya hapo.

“Polisi wanawadanganya Wakenya kwamba wanafanya uchunguzi,’ alisema Musyoka.

Rais Kenyatta anawania urais kwa mara ya tatu baada ya kushindwa na Mwai Kibaki mnamo mwaka wa 2002 na kumshinda Raila Odinga manamo mwaka wa 2013 kwenye uchaguzi uliozua utata na msindi wake kuamriwa na mahakama kuu.

Tayari vifaa vya kupigia kura vimefika katika vingi vya vituo na serikali imetangaza kwamba itatumia maafisa 150,000 kulinda amani wakati wa zoezi hilo.

Wawaniaji wengine wa urais pamoja na wagombea wa nyadhifa mbali mbali pia walifanya mikutano katika maeneo tofauti tofauti na kuwarai wapiga kura kuwachagua. Jumamosi ilikuwa siku ya mwisho ya kufanya kampeni.

Licha ya hali ya wasiwasi kwamba uchaguzi huenda ukagubikwa na ghasia, wachambuzi wametaja kipindi cha kampeni za mwaka huu kama ambacho hakikuwa na visa vingi vya vurugu.

XS
SM
MD
LG